TARI yatafiti mbegu bora zinazokinzana na wadudu, magonjwa, mabadiliko ya hali ya hewa

 

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), inatafiti aina mbalimbali za mbegu zinazokabiliana na wadudu, magonjwa pamoja na mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo ukame, kwa lengo la kuongeza tija katika kilimo.

Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Thomas Bwana amesema hayo katika kilele cha maadhimisho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi jijini Dodoma alipozungumza na waandishi wa habari.

Bwana amesema taasisi hiyo inafanya utafiti huo wa mbegu ili kutatua changamoto zinazowakabili wakulima zinazotokana na magonjwa, wadudu na hali ya hewa.

"Sasa hapa tunakuja kuonyesha aina mbalimbali za teknolojia ambazo tumeziandaa TARI kwa ajili ya kutatua changamoto mbali mbali za wakulima, ikiwa ni pamoja na changamoto za rutuba ya udongo,” alisema Bwana na kuongeza "Pia changamoto za wadudu waharibifu, lakini changamoto za magonjwa.”

"Tuna aina mbalimbali za mbegu bora za migomba, mbegu za jamii ya mikunde lakini tuna mbegu za mpunga, mahindi na korosho," amesema.

Amesema taasisi hiyo imekua ikitafiti mbegu bora ambazo zinakinzana na magonjwa, zenye mazao mengi zaidi ili kuongeza tija kwa wakulima.

"Lakini pia kuna teknolojia nyingine kama ile ya kitalu mkeka hiyo inasaidia kupambana na mabadiliko ya tabia nchi," amesema.

Bwana amesema teknolojia ya kitalu mkeka inawezesha mkulima kupanda mpunga kwa muda mfupi.

"Teknolojia hii ya kitalu mkeka mkulima anaweza kuandaa mbegu hata nyumbani, inasaidia kukimbizana na mvua ambazo zinakua zinabadilika badilika," amesema.

Chapisha Maoni

0 Maoni