Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa misitu
imezindua kampeni ya kupanda miti zaidi ya Bilioni moja katika mikoa ya
kaskazini ili kunusuru barafu ya mlima Kilimanjaro. Kampeni hii ya upandaji
miti inakwenda sambamba na utekelezaji wa mikakati ya kupanda zaidi ya
miti milioni 8 kwa mwaka katika Mkoa wa Kilimanjaro, utoaji elimu kwa umma
kuhusu upandaji miti, na uhifadhi wa mazingira kupitia vipindi vya redio,
televisheni, matamasha na maadhimisho mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Naibu Waziri wa maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula
ameyasema hayo alipokuwa akijibu swali la Mhe. Prof. Patrick Alois Ndakidemi
Bungeni Mjini Dodoma aliyetaka kujua Serikali imechukua hatua gani za muda
mfupi, wakati na muda mrefu kunusuru theluji inayotoweka katika kilele cha
Mlima Kilimanjaro.
Aidha, Mhe. Kitandula alisema kuwa sababu kubwa ya kupungua
kwa theluji katika Mlima Kilimanjaro ni ongezeko la joto duniani kutokana na
mabadiliko ya Tabia nchi yanayochangiwa na ongezeko la shughuli za kibinadamu
hususan ukataji wa miti, kilimo, uchomaji moto katika maeneo yanayozunguka
mlima, uwepo wa mvua chache na vipindi virefu vya ukame, na upepo mkavu kutoka
bahari ya Hindi.
Mhe. Kitandula aliongeza kuwa kwa mikakati ya muda wa
kati Serikali inajielekeza katika kuhimiza matumizi bora ya ardhi na
kuimarisha ulinzi katika maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro na kutekeleza
mipango ya kudhibiti na kupambana na uchomaji moto mlimani.
Aidha, kwa upande wa mikakati ya muda mrefu, Mhe. Kitandula alilieleza bunge kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na mashirika ya kikanda na kimataifa kutekeleza mikakati ya pamoja ya kuhimili na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ikiwa ni pamoja na kuboresha teknolojia za kilimo, kuongeza ufanisi wa matumizi ya maji, kupunguza uzalishaji wa gesi chafu na kurejesha mifumo ikolojia kwenye mlima na maeneo yanayozunguka.
Na. Anangisye Mwateba-Bungeni Dodoma
0 Maoni