Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji
Mstaafu Mhe. Mathew Mwaimu aipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa utoaji wa
elimu ya ubunifu wa mifumo ya utenganishaji taka ambao ni fursa ya ajira.
Mhe. Jaji Mwaimu ametoa pongezi hizo leo Jumatano Julai 7,
2024 wakati alipotembelea banda la Ofisi ya Makamu wa Rais katika maonesho ya
Kitaifa ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja
vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma.
Ameeleza kuwa taka zinazozalishwa nchini kwa sasa zimekuwa
ni fursa kutokana na malighafi hiyo kutumika katika shughuli za uzalishaji mali
na hivyo kuchangia katika ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kuchochea maendeleo
ya kaya, familia na jamii kwa ujumla.
“Taka ni fursa na pia ni vyanzo vya malighafi muhimu katika
shughuli za uzalishaji kutoka. Nawapongeza kwa ubunifu wa utoaji wa elimu
kuhusu fursa zilizopo katika taka kwani mbinu mbadala ya kukuza kipato cha
jamii na kuhamasisha utunzaji wa mazingira” amesema Mhe. Jaji Mwaimu.
Aidha Jaji Mwaimu amewataka wananchi kutumia fursa ya
maonesho hayo kutembelea Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais na kujifunza
teknolojia na bunifu mbalimbali zinazosaidia masuala ya uhifadhi wa mazingira
kwani zipo fursa zinazoweza kusaidia ukuaji wa kipato katika ngazi ya kaya na
jamii kwa ujumla.
Ameongeza kuwa taka ni fursa iliyojificha na hivyo elimu
kuhusu fursa na manufaa yake wananchi wanapaswa kuitambua kwani sio kila kitu
kinachotambulika kama takataka kinatakiwa kutupwa kwenye madampo, bali taka hizo
zinaweza kutumika na kuwa fursa kujipatia kipato.
“Taka zinaweza kuwa fursa endapo zitachambuliwa kuanzia
sehemu ya uzalishaji mpaka mtu wa mwisho anayetumia bidhaa husika, ili kuweza
kuchangamkia fursa hiyo tunatakiwa kujua taka ambazo tunazalisha majumbani na
namna zinavyotakiwa kutenganishwa,” amesema Jaji Mwaimu.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Sarah Kibonde amesema Ofisi hiyo imekuwa ikitumia
mbinu mbalimbali za kuemilisha umma kuhusu masuala ya Muungano na Mazingira
ikiwemo maonesho, mikutano ya wadau na vyombo vya habari.
Ameongeza kuwa katika kupanua wigo wa elimu kwa umma kuhusu
masuala ya Muungano na Mazingira kupitia maonesho hayo, Ofisi ya Makamu wa Rais
imeanisha maeneo matano ya kimkakati kwa ajili ya kuwafikia wananchi na wadau
mbalimbali wanaotembelea banda la ofisi hiyo.
Ametaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na masuala ya nishati
safi ya kupikia, mabadiliko tabianchi, uchumi wa buluu, fursa zitokanazo na
taka, biashara ya kaboni na elimu kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Kupitia maonesho tuna nyaraka mbalimbali ambazo ni vitabu
ikiwemo Kitabu cha Miaka 60 ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mpango Kabambe wa
Kitaifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032), vipeperushi, majarida
ambayo ni mahsusi kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi na wadau nk” amesema
Kibonde.
Ofisi ya Makamu wa Rais imeungana na Wizara, Idara, Taasisi
na Wakala za Serikali na sekta binafsi kushiriki maonesho ya kitaifa ya Sikukuu
ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya
Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma kuanzia tarehe 1-8 Agosti, 2024.
Maonesho hayo yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”.
0 Maoni