Mbunge wa Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde amewapongeza
walimu wanawake wa Dodoma kwa mikakati ya kujiinua kiuchumi na kuchangamkia
fursa za kiuchumi zilizopo mkoani Dodoma.
Mavunde ameyasema hayo wakati akizindua SACCOS ya Walimu
Mkoa wa Dodoma ambayo inaundwa na walimu wa wilaya mbalimbali za Mkoa wa Dodoma
ambayo ina lengo kuu la kusaidia upatikanaji wa mitaji kwa walimu hao wambao
wanashiriki shughuli mbalimbali za kiuchumi.
“Najua jukumu lenu la kwanza ni kufundisha,lakini pia sio
dhambi ninyi kushiriki katika shughuli za kiuchumi ila mradi tu iwe nje ya muda
wako wa kazi na pia kama haiathiri majukumu yako ya msingi ya ufundishaji.”
Nimefurahi sana leo kuona mmeanzisha hii SACCOS maalum kwa
ajili ya walimu kama njia ya uwezeshwaji kiuchumi kwa walimu.
"Nategemea kupitia SACCOS hii itasaidia kupatikana kwa mitaji
ambayo itakuwa chachu ya uanzishwaji wa miradi ya kiuchumi na hasa ikizingatiwa
kwamba kwa sasa Dodoma kuna fursa nyingi za kiuchumi na hivyo ni muhimu
kuzichangamkia mapema,”alisema Mavunde.
Akizungumza katika Hafla hiyo, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa
Dodoma Mh. Fatma Toufiq amepongeza jitihada za walimu wakinamama za kujiletea
maendeleo na kuwataka kuchangamkia fursa mbalimbali za maendeleo na kuahidi
kuwaunga mkono katika shughuli za maendeleo.
Katika hafla hiyo, Wabunge Mavunde na Toufiq wamechangia Tsh
10,000,000 kuiendeleza SACCOS hiyo ya walimu.
Naye muandaaji wa Kongamano la Walimu Wanawake Mkoani
Dodoma, Mwl. Sheila Chinja amesema lengo kuu la kuwakutanisha walimu wanawake
ni kujadili kwa pamoja na kuwaendeleza kiuchumi na ndio maana likaja wazo la
uanzishwaji wa SACCOS hii maalum kwa lengo la kuwawezesha walimu.
Mwl. Sheila pia amemshukuru Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa kwa kuboresha mazingira mazuri ya ufundishaji kwa kuboresha miundombinu ya Elimu.
0 Maoni