Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI (Afya), Mhe. Dkt. Festo
Dugange amekishauri Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji na Usimamizi wa Biashara ya
Kaboni (NCMC) kupanua wigo wa utoaji wa elimu kuhusu fursa na manufaa ya
biashara hiyo kwa wananchi.
Dkt. Dugange amesema hayo jana wakati alipotembelea Banda la
Ofisi ya Makamu wa Rais katika Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima Duniani
(Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini
Dodoma.
Ameongeza kuwa iwapo elimu ya kutosha kuhusu biashara ya
kaboni itatolewa kwa wananchi hususani kupitia fursa ya upandaji miti itasaidia
uelewa kuhusu uhifadhi wa mazingira na kuongeza kipato katika ngazi ya kaya na
jamii kwa ujumla.
Dkt. Dugange amesema zipo baadhi ya Mamlaka za Serikali za
Mitaa zinatekeleza miradi ya biashara ya kaboni na hivyo kutoa ushauri kwa
Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji na Usimamizi wa Biashara ya Kaboni (NCMC)
kubuni na kuweka mipango mahsusi ya kushirikiana na Halmashauri hizo katika
utoaji wa elimu.
“Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) hakina
budi kujitangaza ili kiweze kufahamika na kufikia wadau wengi ikiwezekana hata
kufungua ofisi za Kanda katika Mikoa mbalimbali nchini”.
Amesema ni wakati mwafaka kwa Serikali kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali kuhakikisha elimu ya biashara ya kaboni inatolewa kwani bado
jamii haina hawana uelewa wa kutosha kuhusu kaboni pamoja na fursa na faida
zilizopo katika biashara hiyo.
Naibu Waziri Dugange pia aliitaka Ofisi ya Makamu wa Rais
kupitia NCMC kufanya mikutano na makongamano na wadau ili kutoa elimu kwa
ikiwemo wananchi na taasisi mbalimbali za uwekezaji ambao ndio walengwa wakubwa
wa biashara ya kaboni nchini.
Amesisitiza kwa kuwepo kwa wataalam wengi ambao watasaidia
katika kutoa elimu hiyo ila kwa sasa inaonekana bado kuna uhaba wa wataalamu
kwenye eneo hilo lakini jitihada ikiongezeka basi matunda yake yataonekana kwa
kila mmoja.
Aidha, Dkt. Dugange amezitaka Halmashauri zote nchini
kutenga bajeti kwa ajili ya masuala ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira na
kuhakikisha miti yote inayopandwa inatunzwa na kustawi.
Ofisi ya Makamu wa Rais imeungana na taasisi mbalimbali za umma na binafsi katika maonesho ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yaliyoanza tarehe 1-8 Agosti, 2024 katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma yakiwa na kauli mbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.”
0 Maoni