Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa kwa mujibu wa
takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 jumla ya wapiga kura wapya
5,586,433 wataandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Amesema kuwa wapiga kura hao ni ambao watakuwa wametimiza
umri wa miaka 18 katika kipindi cha kuanzia mwaka 2020 baada ya uchaguzi mkuu
uliopita na ambao watatimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi Mkuu wa Mwaka
2025.
Amesema hayo leo (Jumamosi, Julai 20, 2024) alipozindua
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, katika uwanja wa Kawawa, mkoani
Kigoma. Uzinduzi huo unaashiria kuanza kwa uboreshaji wa daftari la kudumu la
wapiga kura nchi nzima ambapo Mikoa inayoanza uboreshaji wa daftari hilo leo
Julai 20, 2024 hadi Julai 26, 2024 ni
Kigoma, Katavi na Tabora kisha mikoa mingine kufuata.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa taarifa za Tume Huru ya Taifa
ya Uchaguzi, inakadiriwa kuwa wapiga kura 4,369,531 wataboresha taarifa zao.
“Idadi hii si ndogo kwenye zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura hivyo
nitoe rai kwa kila mpiga kura aliyeandikishwa na mwenye uhitaji wa kuboresha
taarifa asisite katika vituo vya kujiandikisha tume imejipanga kuhakikisha
wananchi wote wanafikiwa popote walipo mpaka vitongojini.”
“Nitoe rai kwa kila mpiga kura aliyeandikishwa mwenye
uhitaji wa kuboresha taarifa iwe kwa kurekebisha taarifa au kuhama kutoka eneo
moja la uchaguzi kwenda lingine asisite kufika katika kituo cha kuandikisha
kwani Tume imeshajipanga ili kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa,” amesema
Mhe. Majaliwa.
Aidha, Mhe. Majaliwa amesema kuwa zoezi hilo lina lengo la
kuhakikisha wananchi wote wenye sifa wanapata na kutumia haki yao ya kikatiba
kama ilivyobainishwa kwenye Ibara ya 5 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977.
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amelitaka Jeshi la Magereza
kuweka miundombinu wezeshi ili kuiwezesha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi
kutekeleza wajibu wake wa kuandikisha wafungwa wenye vifungo chini ya miezi
sita na mahabusu kwa ufanisi.
“Hii fursa ambayo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
lilipitisha sheria ya kuwawezesha magereza kupiga kura ya kuchagua viongozi
wanaowataka, hii mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu kutoa fursa kwa
wafungwa na mahabusu kupiga kura wakiwa magerezani,” amesema Mhe. Majaliwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewahakikishia
watanzania kuwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuhakikisha kuwa
chaguzi zote zitakuwa huru na Haki.
Kwa Upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Bunge na Uratibu) Ummy Nderiandanga amesema kuwa uzinduzi wa uandikishaji na
uboreshaji, mchakato huo umeshirikisha wadau mbalimbali wa uchaguzi ikiwa ni
utekelezaji wa falsafa ya 4R za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Tume imekutana na wadau wa makundi mbalimbali kama vile
Vyama vya Siasa, Asasi za Kiraia, Viongozi wa Dini, Makundi Maalum kama vile
Vijana, Wanawake na watu wenye Ulemavu . Lengo ni kuhakikisha kuwa mchakato huu
unakuwa shirikishi kwa watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vya siasa
au dini.”
Naye, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji
Jacobs Mwambegele amesema kuwa Jumla ya vituo 40,126 vitatumika katika zoezi la
uboreshaji wa Daftari ambapo kati ya hivyo, vituo 39,709 vipo Tanzania Bara na
vituo 417 vipo Tanzania Zanzibar.
“Idadi hii ya vituo ni ongezeko la vituo 2,312 zaidi
ikilinganishwa na vituo 37,814 vilivyotumika kuandikisha Wapiga Kura kwa mwaka
2019/2020.”
Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akimkabidhi kadi ya kupigia kura makazi wa Kigoma alipozindua uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, katika uwanja wa Kawawa, mkoani Kigoma.
0 Maoni