Wananchi wahimizwa kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii Sabasaba

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abass, amewahimiza wananchi kutembelea maonesho ya 48 ya Kimataifa SABASABA, na kujionea shughuli mbalimbali za uhifadhi wa maliasili na utalii zinazofanywa na wizara pamoja na taasisi zake.

Dkt. Abbas ameyasema hayo leo jana, alipotembelea maonyesho hayo jijini Dar es salaam, ambapo miongoni mwa mabanda aliyotembelea ni Banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania - TFS.

Akizungumza mara baada ya kupita kwenye banda la TFS na wadau wake, Dkt. Abbas amesema Wizara na Taasisi zake zipo katika maonesho hayo ya Sabasaba pamoja na mambo mengine zinatoa  elimu kwa wananchi kuhusu uhifadhi wa rasilimali misitu ambao kupitia TFS nchi sasa imeshuhudia kuongezeka kwa kasi ya uwekezaji wa mazao mapya ya utalii ikolojia, ufugaji nyuki na mazao yake.

"Leo nipo hapa kwenye Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii na kazi kubwa tunazoendelea nazo hapa ni mbili, kwanza tunaonesha uhifadhi ambapo wananchi wanakuja kujifunza na kuona namna nchi yetu imewekeza katika uhifadhi wa misitu, ufugaji nyuki na wanyamapori, na mchango wake kwenye pato la Taifa ."

"Eneo la pili kubwa kwenye banda letu ni kuweza kuona shughuli mbalimbali kwenye utalii kama mnavyofahamu Taifa letu linafanikiwa sana katika maeneo ya utalii kwa sasa na tangu Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan afanye Royal Tour watalii wengi wamekuwa wakiongezeka wa ndani na wa nje ya nchi yetu, hivyo banda letu litakuwa wazi na tunaomba wananchi waje kujionea shughuli mbali mbali za uhifadhi pamoja na wanyamapori, " amesema.

Ameongeza kuwa wananchi watakaotembelea Banda la Maliasili na Utalii wataweza kuona namna nchi inavyohifadhi maliasili za nchi lakini pia watanufaika na ofa mbalimbali za kutembelea vivutio vya utalii kwenye misitu ya hifadhi na hifadhi za Taifa.

"Sasa hivi tuna Utalii wa Ikolojia unaofanyika kwenye maeneo ya misitu, zamani tulizoea utalii wa wanyama lakini kwa sasa wananchi wamezoea kwenda kwenye maeneo ya misitu na kupata hewa safi, yanajengwa mahoteli, wanapumzika, kuna maporomoko ya maji na madhari nyingine nzuri, na hivyo mfano mzuri ni hapahapa Dar es Salaam kwenye msitu wetu wa Pugu Kazimzumbwi uliopo Kisarawe mkoani Pwani kuna bwawa pale kubwa watu wanapanda ngalawa,viboti vidogo wanavinjali wanaondoa stress," amesema Dkt. Abbas.

Ameendelea kusema kuwa watakapotembelea banda la TFS watajionea pia zao la asali na mazao yake, watapata mbegu bora, miche ya matunda na miche ya miti ya kibiashara kwaajili ya kujipatia kipato.

Hata hivyo ameendelea kuwakaribisha wananchi na wadau mbalimbali kuwekeza katika sekta ya utalii kwa kile alichosema kuna fursa nyingi kama vile ujenzi wa hoteli na kambi mbalimbali.

                       Maonesho haya ya 48 ya Biashara ya Kimataifa yanaendelea hadi tarehe 13 Julai 2024

Chapisha Maoni

0 Maoni