Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anasisitiza ufanyaji kazi kwa
ushirikiano kati ya Serikali na Taasisi za Dini (Kidini) nchini ili kuendelea
kujenga amani, umoja na mshikamano.
Amesema kuwa Serikali
inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Taasisi hizo ambao huleta matokeo chanya
kwa ustawi wa Taifa.
“Tunashukuru tunapata
ushauri, yapo mambo ambayo mnayafanya na kuiwezesha nchi hii iendelee,
mshikamano wetu ndani ya nchi, umoja wetu ndio unaozaa utulivu na amani
tuliyonayo.”
Amesema hayo wakati akiwasilisha Salamu za Pongezi kutoka
kwa Rais Dkt. Samia leo (Jumatano, Julai 03, 2024) kwa Rais wa Baraza la
Maaskofu Tanzania (TEC) Mhashamu Wolfgang Pisa ambaye pia ni Askofu wa Jimbo
Katoliki la Lindi, kwenye makazi ya Askofu, Mtanda mkoani Lindi.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kumpa ushirikiano wa dhati
“wakati wote utakapokuwa na jambo ambalo unadhani Serikali inahitaji kushauriwa
uwe huru na wakati wote unapoona kwamba unahitaji kuunganisha nguvu na
Serikali, sisi tutakupa ushirikiano.”
Ameongeza kuwa Serikali kwa upande wake imeshaagiza
ushirikiano huo usiwe tu ngazi ya kitaifa bali uende hadi katika ngazi ya
vitongoji “Tuendelee kuwa pamoja na kuja kwangu hapa nikuhakikishie tunaendelea
kukupa ushirikiano.”
Kwa upande wake Askofu Pisa amemshukuru Rais Dkt. Samia Kwa
salamu za pongezi za kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa TEC.
Uchaguzi wa viongozi wapya wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) uliohusisha nafasi za Rais, Makamu wa Rais na Katibu ulifanyika tarehe Juni 21, mwaka huu, ambao waliochaguliwa ni Mhashamu Wolfgang Pisa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi (Rais), Mhashamu Eusebius Nzigilwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda (Makamu wa Rais) na Padre Charles Kitima Padre wa Jimbo Katoliki la Singida (Katibu Mkuu).
0 Maoni