Ushirikiano wa Tanzania, Ireland umeongeza kasi usawa wa kijinsia - Dkt. Gwajima

 

Utekelezaji wa programu za Jinsia na wanawake zilizotekelezwa na Serikali ya Ireland kwa ushirikiano na Tanzania umechangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza usawa wa kijinsia, ushirikishwaji wa kijamii na kushughulikia ukatili wa kijinsia.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameyasema hayo akizungumza na Balozi wa Ireland nchini Tanzania aliyemaliza muda wake Mhe. Mary O'Neil jijini Dar es Salaam Julai 26, 2024.

Waziri Dkt. Gwajima ameeleza kwamba, utekelezaji wa mipango ya Jinsia na uwezeshaji Wanawake chini ya ushirikiano wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania umesaidia kwa kiasi kikubwa kuwezesha utekelezaji wa Vipaumbele vya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi. 

Amempongeza balozi huyo kwa uhusiano mzuri na Serikali ya Tanzania kwa kuzingatia kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Ubalozi wa Ireland, na wadau wote wa usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.

"Wakati wa mamlaka yako kama Balozi wa Ireland nchini Tanzania, tumeshuhudia kazi yako muhimu katika kukuza usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake na michakato ya sera na sheria," amesema Waziri Dkt. Gwajima. 

Ameainisha baadhi ya kazi zilizofanywa na Balozi huyo ni pamoja na kushiriki katika kuongeza uwezo wa utekelezaji wa mikakati ya maendeleo endelevu (SDG), kujenga uwezo wa hospitali ya CCBRT kuhudumia wenye ulemavu pamoja na wanawake wenye tatizo la fistula,  kushiriki kwenye kuwezesha mfuko wa Afya Ili kuimarisha afya ya msingi, kuhuisha sera ya maendeleo ya Jinsia, uwezeshaji wanawake kiuchumi na programu ya mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na kwa watoto.

Kwa upande wake Balozi O'Neil amesema kupitia ushirikiano wa Tanzania na Ireland mambo mengi yamefanyika ikiwemo SIGI report (Social Institutions and Gender Index), mikakati kuelekea utekelezaji wa Ulinzi na Usalama kwa wanawake hivyo, atahakikisha anamkabidhi Balozi ajaye yale yote yanayotakiwa kuendelezwa hasa uwezeshaji wanawake kiuchumi Ili aendelee na kazi.

Na WMJJWM- Dar es Salaam

Chapisha Maoni

0 Maoni