Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
amesema anafurahishwa na namna makada, wanachama na viongozi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. Samia Suluhu Hassan, wanavyoendeleza umoja miongoni mwao.
Rais mstaafu Dkt. Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti Mstaafu
wa CCM, amesema umoja miongoni mwa wanachama ndio nguzo na silaha muhimu hasa
wakati huu wa kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa
mwakani.
Kiongozi huyo mstaafu amesema hayo jana, alipokutana na
kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi
aliyemtembelea kumjulia hali kwenye ofisi yake binafsi, jijini Dar Es Salaam.
Rais Mstaafu Kikwete ametumia nafasi hiyo kumwambia Balozi
Nchimbi kwa jinsi anavyofurahishwa na namna maelekezo anayotoa Mwenyekiti wa
CCM Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuwataka viongozi wa Chama kushuka chini kwa
wanachama na wananchi kwa lengo la kuwasikiliza na kutatua kero zao, yanavyotekelezwa
kikamilifu.
Aidha, Rais Mstaafu Kikwete ameipongeza sekreterieti mpya ya
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa jinsi inavyojikita katika kuimarisha chama
na kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya 2020 -2025 kwa wananchi.
“ Umoja na mshikamano wa wana-CCM ndiyo umekuwa siri na
silaha ya ushindi wa CCM, ndiyo maana tunasema siku zote umoja wetu ndiyo
ushindi wetu. Tunafurahia sana tunavyoona wana-CCM chini ya uongozi wa
Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt
Samia Suluhu Hassan wanaendeleza kuimarisha msingi huo. Hongereni sana ,"
amesema Rais Mstaafu Kikwete.
Kwa upande wake, Balozi Dkt. Nchimbi amewashukuru viongozi
wastaafu wa Chama na Serikali kwa jinsi wanavyofanya kazi ya kuwalea kiuongozi
na kimaadili viongozi wa sasa.
Balozi Dkt. Nchimbi amesema CCM itaendeleza utamaduni wa
kuwaenzi na kuwasikiliza viongozi wastaafu
Balozi Nchimbi amesema kwa uzoefu wa uongozi na kazi nzuri ya kulitumikia taifa waliyofanya wakati wa uongozi wao, viongozi hao ni hazina kubwa kwa kizazi cha sasa na kijacho.
0 Maoni