Mhe. Kitandula akemea ucheleweshwaji taarifa za tathmini ya madhara ya wanyama wakali na waharibifu

 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula amekemea vikali tabia ya baadhi ya watumishi wa umma kuchelewa kufikisha Wizarani kwa wakati taarifa za tathmini ya athari wanazopata wananchi kutoka kwa wanyama wakali na waharibifu. Mhe. Kitandula alisema ucheleweshwaji huo wa taarifa unasababisha wananchi kuchelewa kupata kifuta jasho na machozi kwa wakati.

Mhe. Naibu Waziri ameyasema hayo kwa nyakati tofauti akiwa kwenye ziara ya kikazi katika wilaya za Ruangwa na Liwale mkoani Lindi kwa lengo la kukutana na wananchi na kuelezea jitahada zinazifanywa na serikali kudhibiti changamoto ya wanyama wakali na waharibifu.

Mhe. Kitandula aliongeza kuwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo, taarifa za tathimini zinapaswa kufikishwa Wizarani ndani ya siku saba baada ya majanga kutokea; lakini kwa sasa madai huchukua muda mrefu kufikishwa wizarani na hivyo kufanya mchakato mzima kuchukua muda mrefu kushughulikiwa.

Vilevile akiwa wilayani Liwale, alizitaka serikali za vijiji wilayani humo kudhibiti ufugaji holela kufanyika kwenye maeneo yao ya vijiji, na kushauri kuwa wafugaji wenye makundi makubwa ya ng’ombe waelekezwe kwenda kwenye maeneo maalum yaliyotengwa na Halmadhauri kwaajili ya ufugaji. Tusiwaache wafugaji waingize mifugo yao kwenye mapori na hifadhi kufanya uharibifu wa vyanzo vya maji na mazingira wanayoishi  wanyamapori kwani kwa kufanya hivyo kunawafanya tembo kuja kutafuta maji na chakula  kwenye makazi ya watu.

Aidha Mhe. Kitandula aliongeza kuwa serikali inatambua changamoto iliyopo ya wanyama wakali na waharibifu na kwamba serikali itafanya kila linalowezekana kudhibiti hali hiyo, na alitumia fursa hiyo kutoa pole kwa wananchi wanaokabiliwa na changamoto hiyo.

Mkuu wa wilaya ya Ruangwa Mhe. Hassan Ngoma akimshukuru Naibu Waziri ameahidi  kuchukua hatua kwa watendaji ambao hawatimizi wajibu wao wa kufanya tathimini ya majanga ya wanyama wakali na waharibifu kwa haraka, lakini pia alimuahidi kuwasimamia kwa ukaribu askari wa uhifadhi ambao wataletwa kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Liwale Mhe. Goodluck Mlinga na Mbunge wa Liwale Mhe. Kuchauka waliishukuru Wizara ya Maliasili na utalii kwa kuitengea wilaya hiyo mabomu baridi 700 kwaajili ya kutumika kudhibiti tembo wilayani Liwale. Aidha waliiomba wizara kuona uwezekano wa kuongeza askari wa uhifadhi katika wilaya hiyo ambayo inaeneo kubwa ambalo ni zaidi ya asilimia 50 ya eneo lote la mkoa wa Lindi.

Na. Anangisye Mwateba-Lindi

Chapisha Maoni

0 Maoni