Dk. Mwigulu ampa rungu Kamishna Mkuu mpya wa TRA

 

Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba amesema kuwa bado kuna watumishi wachache wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao si waadilifu na kumtaka Kamishna Mkuu wa TRA kuwachukulia hatua za kuwafukuza kazi.

“Bado kuna baadhi ya watendaji wachache wa TRA katika baadhi ya maeneo ambao wanagawana fedha za mapato na serikali, wanachukua sehemu ya mapato na kuwasilisha serikalini fedha pungufu,” alisema Dk. Mwigulu na kuongeza, “Watumishi wa aina hiyo Kamishna Mkuu wa TRA wanapaswa kuchukuliwa hatua ya kufukuzwa kazi wasiwepo kabisa serikalini, sisemi mwende mkawaonee lakini mkatende haki.”

Dk. Mwigulu ametoa kauli hiyo kwenye Kikao Kazi cha Nane cha Mamlaka ya Mapato Tanzania, kilichohudhuriwa na watendaji wakuu wa TRA nchi nzima chini ya Kamishna Mkuu mpya wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda.

Hata hivyo, Dk. Mwigulu amewatia nguvu watumishi wa TRA, kwa kuwataka kwenda kukusanya kodi kwa uadilifu na kuzingatia sheria, huku akiwaeleza bayana kuwa anajua kwamba kazi ya kukusanya mapato ni kazi ngumu.

“Kukusanya mapato ni kazi ngumu sana, na mara zote kazi ya kukusanya mapato ni kazi ya lawama tu, haijaanzia sasa nakumbuka hata Zakayo alisemwa na hata ambaye halipi kodi, hata sasa wasiolipa kodi ndio wanaopiga kelele na hata wale ambapo wanaokwepa kodi,” alisema Dk. Mwigulu.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu mpya wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda alieleza kuwa katika kikoa hiyo wamefanya tathimini ya utendaji kazi wa TRA kwa mwaka jana na kutengeneza mikakati ya kuhakikisha wanakusanya mapato ya sh trilioni 30.4.

Chapisha Maoni

0 Maoni