Serikali ipo imara na itaendelea kuwatumikia- Majaliwa

  

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo imara na inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo, hivyo waendelee kuipa ushirikiano.

"Serikali yenu inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ili kuwawezesha wananchi wake kufanya shughuli za kimaendeleo. Miradi hii ni ile ya huduma za kijamii ambayo Watanzania, Wanakatoro kila siku lazima iwaguse. Serikali imejikita hapo.”

Amesema hayo jana Juni 02, 2024 wakati akizungumza na wananchi katika Mji Mdogo wa Katoro, Geita. Amesema utekelezaji wa miradi hiyo utawawezesha wananchi kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kushiriki katika shughuli za kujiingizia kipato.

Waziri Mkuu amesema kwa sasa Serikali itaongeza fedha kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa madarasa ili kuwezesha  idadi ya vyumba vya madarasa viendane  na  idadi  ya  wanafunzi na   kuwa na uwiano mzuri. “Kutokana na idadi kuwa ya watu hapa Katoro tumekusudia kuongeza vyumba vya madarasa ili kupunguza msongamano madarasani.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemuagiza Kamanda wa Polisi wa wilaya ya Geita ahakikishe analitokomeza kundi la kihalifu maarufu mazombi ambayo yamekuwa yakiwasumbua wananchi kwa kuwapora mali zao.”Hatuhitaji kuwa na mazombi hapa.”

Pia, Waziri Mkuu ameziagiza kamati za mazingira katika vijiji vyote zihakikishe maeneo yote ya vyanzo vya maji yanalindwa na kuzuia shughuli za kibinadamu zikiwemo za kilimo, ufugaji na ukataji wa miti ili kuepusha taifa kugeuka jangwa.

Awali, Mbunge wa Busanda, Tumaini Mageza aliishukuru Serikali kwa kuimarisha huduma za kijamii katika jimbo lao ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama ambapo hadi sasa tayari nyumba zaidi ya 200 zimeshaunganishiwa maji na vituo 10 vya kuchotea maji vimeanzishwa.

Mbunge huyo alitumia fursa hiyo kuomba Serikali ianzishe mradi wa ujenzi wa shule za msingi za ghorofa kwa kuwa katika mji huo wanazaliwa watoto wengi kwa mwezi watoto 1,000 hivyo wakiendelea kujenga shule za kawaida watakosa maeneo.

Chapisha Maoni

0 Maoni