FORVAC yasaidia jamii kuzalisha Sh Bilioni 9 kwa mazao ya misitu

 

Mradi wa Uongezaji Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC) umezisaidia jamii nchini kuzalisha Euro milioni 4 (Shilingi bilioni 9 za Tz) kutokana na matumizi endelevu ya misitu, huku 60% ya fedha hizo zikienda kwenye huduma za kijamii kama vile shule, zahanati pamoja na ongezeko la mapato kutoka kwenye miti iliyosindikwa kwenye Halmashauri 5 za Mradi huo.

Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi alipokuwa akifungua Kikao cha Bodi ya Usimamizi na Kamati ya Uongozi ikiwa ni kikao cha mwisho mradi huu unaotarajiwa kukamilika mwezi Julai 2024.

Pia, amesema kuwa kupitia mradi huo, takribani Hekta 460,000 za misitu sasa ziko chini ya udhibiti wa jamii na usimamizi endelevu.

Aidha, amefafanua kuwa Serikali iko katika hatua za mwisho za kuandaa mradi mpya wa thamani ya takribani shilingi bilioni 50 utakaojulikana kama - Misitu, Matumizi ya Ardhi na Mpango wa Kukuza Minyororo ya Thamani - (FORLAND) utakaolenga kuendeleza na kuimarisha mafanikio mengi yaliyopatikana kupitia miradi ya FORVAC na Panda Miti Kibiashara (PFP).

Kikao hicho kimehudhuriwa na Mwenyekiti mwenza, Mhe. Theresa Zitting ambaye pia ni Balozi wa Ufini nchini Tanzania.

Chapisha Maoni

0 Maoni