Chuo Kikuu Huria chamlilia Dkt. Shogo Mlozi

Shairi la kumlilia Dkt. Shogo Mlozi-Sedoyeka aliyefariki tarehe 13 Juni, 2024 katika Hospitali ya Mount Meru jijini Arusha. Dkt. Shogo aliwahi kuwa mhadhiri na Mkuu wa Idara katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika Idara ya utalii na ukarimu na baadae akateuliwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii na baada ya muda kidogo akachaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika ya Mashariki mpaka umauti ulipomkuta.

KIITIKIO 
Nyoyo'ze zasikitika, machozi hayakatiki
Ni kutwa kububujika, machoni hapakauki
Muumba wetu Rabuka, E-Mungu mwenye miliki
Mpokee Dokta. Shogo, OUT twamuombea.

1
OUT yote yalia
Nyoyo'zo zimezimia
Huzuni imewaingia
Dkt. Shogo kawaumiza

2
Utalii mtalamu
Mpole mtu rahimu
Heshima na ukarimu
Sifa'ze Dokta Shogo

3
Cheko lake tabasamu
Ni sifa'ye maalumu
Hata umpime damu
Shogo kajawa upendo

4
Uhadhiri ualimu
Shogo alizihudumu
Kuifundisha kaumu
Ya Huria Tanzania

5
Ta'mkumbuka dawamu
Mlozi mwenye nidhamu
Kwa Mungu wetu Rahimu
Peponi ataingia

6
Profesa Sedoyeka
Pole sana ya hakika
Mke wako kuondoka
Mwenyezi akupe nguvu

7
Na watoto kadhalika
Pole zetu ziwafika
Wazazi na marafika
Poleni sana msiba

8
Pole na kwako Spika
Na wote waheshimika
Wa Bunge la jumuika
Afrika ya Mashariki 

KIITIKIO 
Nyoyo'ze zasikitika, machozi hayakatiki
Ni kutwa kububujika, machoni hapakauki
Muumba wetu Rabuka, E-Mungu mwenye Miliki
Mpokee Dokta Shogo, OUT twamuombea

MTUNZI 
DKT. Mohamed Omary Maguo
Mshairi wa Kisasa
Mhadhiri Mwandamizi
Mkuu wa Itifaki

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania


Chapisha Maoni

0 Maoni