Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii imewasili katika Wilaya Mbarali, Mkoani Mbeya kuratibu zoezi maalumu la kuwaondoa tembo kwenye makazi ya watu katika kata tano za Igava, Mawindi, Miyobweni, Imalilosongwe na Rujewa ambapo zoezi litaanza katika vijiji vya Kata ya Igava ambavyo vimeathiriwa zaidi na uvamizi wa tembo.
Akizungumzia zoezi
hilo , Mwakilishi wa Wizara
ya Maliasili na
Utalii Antonia Raphael
amesema zoezi hilo litafanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia tarehe 08 hadi 09 Mei, 2024 ambapo teknolojia ya
helikopta itatumika kuwaswaga
tembo hifadhini sambamba na kuwafunga
mikanda maalum ya mawasiliano
(GPS satellite Collars) tembo viongozi wa makundi ili kufuatilia
mienendo yao.
Vilevile, Anthonia
amesema kuwa zoezi hilo litaongozwa na Mheshimiwa waziri
wa Maliasili na Utalii.
Naye, Dkt. Emmanuel
Masenga ambaye ni
Mtafiti Mkuu kutoka Taasisi ya Utafiti
wa Wanyamapori Tanzania
(TAWIRI) amebainisha kuwa maandalizi
ya zoezi hilo yamekamilika ambapo
timu ya wataalamu kutoka Wizara ya
Maliasili na Utalii na taasisi
zake za TAWIRI, TANAPA, TAWA
pamoja na timu kutoka Wilaya ya
Mbarali zipo uwandani kuhakikisha zoezi
la kuwaondoa tembo kwenye makazi ya watu linaanza kesho kwa ufanisi.
Dkt. Masenga amesema teknolojia ya helikopta
imekuwa na manufaa katika
kuwaondoa tembo kwenye makazi ya watu kwa haraka zaidi.
Naye, mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Donald Mwigombe ambaye pia ni Afisa Tarafa ya Rujewa, ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari wakati wa zoezi la kuwaswaga tembo kutoka kwenye makazi ya watu ambapo amewataka wananchi kutokusogea karibu na tembo, wakati zoezi linaendelea ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na tembo pindi wanaposwagwa kwa helikopta.
0 Maoni