Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kuwa
uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kwahani lililopo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini
Magharibi, Zanzibar utafanyika tarehe 08 Juni, 2021.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na kusainiwa na Mkurugenzi wa
Uchaguzi wa INEC, Bw. Kailima, R. K jijini Dodoma jana, imesema kwamba fomu za
uteuzi kwa ajili ya uchaguzi huo mdogo zitatolewa kuanzia tarehe 17 hadi 23
Mei, 2024.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa uteuzi wa wagombea utafanyika
tarehe 23 Mei, 2024 na kampeni kwa ajili ya uchaguzi huo zitafanyika kuanzia
tarehe 24 Mei, 2024 hadi tarehe 07 Juni, 2024.
Tume imetangaza uchaguzi huo mdogo kufuatia taarifa ya Spika
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyomtaarifu Mwenyekiti wa Tume
kuhusu uwepo wa nafasi wazi ya ubunge katika Jimbo la Kwahani.
Spika ametoa taarifa hiyo kwa kuzingatia matakwa ya kifungu
cha 49(2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka,
2024.
“Kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 49(1)(b) cha Sheria
ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, Tume inatoa
taarifa kwa umma kuhusu uwepo wa uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la
Kwahani lililopo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar,” imesema
sehemu ya taarifa hiyo.
Tume imevikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Katiba, sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo ya Tume katika kipindi cha uchaguzi huo mdogo.
0 Maoni