Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel
John Nchimbi, amesema kazi kubwa inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, ndiyo siri na chachu ya chama na
viongozi wake katika kuwatumikia wananchi.
Balozi Dk. Nchimbi ameongeza kusema kuwa katika kutekeleza
kwa vitendo Falsafa ya 4R ya Mhe. Rais Samia na kuwatumikia wananchi
waliokipatia dhamana ya kuongoza, CCM kikiwa Chama kiongozi nchini, kitaendelea
kutimiza wajibu wake wa kuwaunganisha Watanzania kuwa wamoja wenye mshikamano
bila kubaguana kwa kuangalia maeneo wanayotoka, dini, kabila wala itikadi za
kisiasa.
Balozi Dk. Nchimbi, ameyasema hayo wakati wa mazungumzo kati
yake na Katibu Mkuu wa Chama Tawala cha Burundi, CNDD – FDD, Mhe. Révérien Ndikuriyo,
yaliyofanyika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba, jijini Dar Es
Salaam, leo Ijumaa, Mei 3, 2024.
“Asante kwa pongezi zako za utekelezaji wa ilani ya CCM.
Mojawapo ya nguzo za uimara wa CCM ni pamoja na kazi kubwa sana zilizofanywa na
Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka hii
mitatu. Zinatupatia ujasiri na jeuri ya kuwa barabarani, kwenda kuzungumza na
wananchi kwa sababu tunayo mambo ya kusema na kuonesha. Na wananchi wanatuunga
mkono.
“Lakini pia katika uhusiano kati yetu, CCM tunafurahi sana
jinsi ambavyo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Burundi,
Mheshimiwa Évariste Ndayishimiye ni marafiki. Hivyo vyama vyetu ni marafiki,
nchi zetu ni rafiki na hata viongozi wetu ni marafiki, ni wajibu wetu sisi
tuendelee kuenzi na kulinda uhusiano na ujirani wetu mwema, kwa ajili ya watu
wetu wa pande zote mbili,” amesema Balozi Dk. Nchimbi.
Kwa upande wake Mhe. Ndikuriyo amesema kuwa CCM na Tanzania
kwa ujumla, ni sehemu muhimu kujifunza kwa ajili ya kujiimarisha, hususani
wakati huu ambapo Chama cha CNDD – FDD kinaendelea kuisimamia Serikali ya
Burundi katika kulinda misingi ya demokrasia inayotokana na utashi wa Warundi.
Katika ujumbe wake, Mhe. Ndikuriyo aliambatana na Balozi wa Burundi nchini Tanzania, Mhe. Leontine Nzeyimana na maofisa wengine wa Chama cha CNDD- FDD kutoka Burundi.
0 Maoni