Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imepitisha Kanuni za Tume
Huru ya Taifa ya Uchaguzi za Mwaka 2024 na Kanuni za Uboreshaji wa Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura za Mwaka 2024 ikiwa ni hatua muhimu katika kuzitafsiri
sheria zilizotungwa na Bunge hivi karibuni.
Sheria zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania zinazohusu uchaguzi ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani
Na. 1 ya Mwaka 2024 na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka
2024.
Kanuni hizo zilizopitishwa leo tarehe 11 Mei, 2024 kwenye
kikao cha Tume kilichofanyika Mjini Unguja, Zanzibar pia zinatoa mwongozo wa
namna ya utekelezaji wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
ikiwa ni maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Baada ya kupitishwa kwa kanuni hizo, hatua inayofuata ni
kuzichapisha kwenye gazeti la serikali ili ziweze kutumika rasmi ambapo kwa
mujibu wa Tume, Kanuni hizo zitachapishwa tarehe 17 Mei, 2024.
Kanuni hizo zimepitishwa baada ya kuandaliwa na wataalamu na
kupelekwa kwa wadau kwa ajili ya kutoa maoni yao ambayo yamefanyiwa kazi na
kujumuishwa kabla ya kupitishwa na Tume.
Wadau waliotoa maoni yao ni pamoja na Vyama vya Siasa, Taasisi za Dini, Serikali, Taasisi za Umma, Mahakama, Asasi na Taasisi zisizo za Kiserikali, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu.
Na. Mwandishi Wetu- Zanzibar
0 Maoni