Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Mwanjelwa Jijini Mbeya
wametakiwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuzuia, kudhibiti na kutokomeza
uhalifu katika Jiji hilo.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Abdi Issango Mei 07, 2024 wakati
akizungumza kwenye kikao na viongozi na wafanyabiashara wa Soko Kuu la
Mwanjelwa.
Kamanda Issango amesema kuwa, Jeshi la Polisi linathamini
mchango mkubwa unaotolewa na wafanyabiashara hivyo litaendelea kuhakikisha
ulinzi na usalama unaimarishwa katika maeneo yao ya biashara ili kukuza uchumi
na kipato.
Aidha, Kamanda Issango amesisitiza wafanyabiashara hao kufanya
kazi kidigitali kwa kuhakikisha wanafunga kamera za usalama (CCTV) kwenye
maduka yao ili kuzuia uhalifu na pindi unapotokea kurahisisha kazi ya
upelelezi.
Naye, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mbeya
Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Andrew Kantimbo amewataka wafanyabiashara wa
Soko Kuu la Mwanjelwa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kwenda kutoa
ushahidi mahakamani badala ya kudai kurejeshewa mali zao na kuomba kutoendelea
na kesi hali inayopelekea watuhumiwa kuachiwa na kurudi mitaani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Mbeya Kamishna
Msaidizi wa Polisi (ACP) Anthony Mkwawa amewataka wafanyabiashara hao
kushirikiana na Polisi Kata waliopo katika maeneo yao na kuunda vikundi vya
ulinzi shirikishi ambapo vitafanya doria kwa lengo la kuzuia uhalifu.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wengine ndugu
Emmanuel Ndanta amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Jeshi la Polisi hasa
ushirikiano toka kwa Polisi Kata na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mwanjelwa Mrakibu
Msaidizi wa Polisi (ASP) Christina Kakiziba pamoja na Askari wengine kwani
umesaidia kuzuia vitendo vya uhalifu hasa uporaji na uvunjaji wa maduka.
Mbali na kutoa elimu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilipata nafasi ya kusikiliza kero na changamoto toka kwa wafanyabiashara hao kwa lengo la kuboresha utoaji huduma bora kwa mteja na kuimarisha ulinzi na usalama katika mazingira yao ya kazi.
0 Maoni