Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amewashauri wachungaji kuwa na maono makubwa katika kuongoza waumini
katika makanisa yao ili kujenga Taifa la watu wenye mwelekeo chanya.
Akizungumza jana Jijini Dodoma wakati wa kufunga kikao cha
mazungativu (Retreat) kwa wachungaji wa Kanisa la FPCT, Dkt. Biteko amesema
kuwa ili waumini wapate uelekeo wa kwenda mahali fulani, wanahitaji mtu mmoja
miongoni mwao atakaye waongoza kufikia malengo waliyojiwekea kutokana na maono
aliyonayo.
“Wachungaji msihangaike na wingi wa watu mahali popote,
angalia uwezo wa kiongozi anayeona mbali atawaongoza wafike mbali,” amesema
Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa “ Askofu Mkuu umechagua fungu jema kufanya
wachungaji hawa wakutane hapa
kujiongezea maarifa kwa kuwa tuko katika dunia iliyojaa utandawazi
na mafundisho ya kweli na yasiyo ya kweli. Ni vigumu kwa
waumini kutambua ya kweli na yasiyo ya kweli
hivyo, wanahitaji kuongozwa”.
Aidha, Dkt. Biteko amewahimiza viongozi wa dini kuwaongoza waumini kiroho na
kuchagua viongozi sahihi wanaofahamu kuwa
watawaletea maendeleo na ustawi
wa nchi.
Pia, amewaomba viongozi wa dini kuwahimiza waumini kufanya
kazi kwa bidii, kuhubiri kuhusu amani pamoja na kusisitiza maadili kwa waumini.
Dkt. Biteko ametaja mafanikio mbalimbali ya Serikali
inayoongozwa na Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, huku akiwaomba wachungaji hao
kuendelea kumuombea na kumtia moyo ili aendelee kutekeleza miradi ya nchi
katika maeneo mbalimbali.
“ Mradi wa reli ya kisasa (SGR) ni mradi mkubwa haikuwa
rahisi kupata fedha za kutekeleza mradi huu lakini Rais Samia amefanikiwa,
Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Julius
Nyerere unaozalisha megawati 2115 umefanikiwa, Pia Serikali imejenga
madarasa, zahanati, vituo vya afya na kutoa ajira kwa watumishi wa sekta ya
afya, angalieni nia yake, muungeni mkono”, amebainisha Dkt. Biteko.
Vilevile, amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa dini na
imani za watu hivyo viongozi wa dini wahimize waumini kuchagua viongozi
wanaofaa.
“Mwaka huu tuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa, viongozi wa
dini mna uwezo wa kuwahamasisha waumini waweze kuchagua viongozi wanaowahitaji
kwa ajili ya kuwaletea maendeleo”, amesisitiza Dkt. Biteko.
Naye, Askofu Mkuu wa FPCT, Steven Mulenga amesema kuwa lengo
la semina hiyo ya siku nne kwa wachungaji ni kuwajengea uwezo watumishi wa
Mungu namna ya kumkaribisha Yesu Kristo.
“Haya tuliyofundishana yatakuwa na matokeo kwa nchi ya
Tanzania”, amesema Askofu Mulenga.
Semina hiyo wa wachungaji FPCT imehudhuriwa na wachungaji kutoka nchi za Kenya, DRC, Rwanda na Sudani Kusini.
CHANZO: Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu
0 Maoni