WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kati ya Julai, 2023 na
Januari, 2024 Serikali imefanikiwa kukusanya sh. trilioni 17.1 ambazo ni sawa
na asilimia 95.9 ya lengo la kukusanya sh. trilioni 17.9.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Aprili 3, 2024), wakati akiwasilisha
Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2023/2024 na
Mwelekeo wa Kazi zake kwa mwaka 2024/2025 Bungeni, jijini Dodoma.
“Katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Januari, 2024 mapato ya
ndani yakijumuisha mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa yalifikia shilingi
bilioni 17,188.4, sawa na asilimia 95.9 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni
17,929.8 na ukuaji wa asilimia 10.0 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka
2022/2023.”
Amesema kati ya mapato hayo, sh. bilioni 15,159.8, sawa na
asilimia 97.9 ya lengo la kukusanya sh. bilioni 15,492.7 zilikusanywa na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) huku Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala na
Taasisi za Serikali zikikusanya sh. bilioni 1,374.5, sawa na asilimia 78.2 ya
lengo la kukusanya sh. bilioni 1,758.3. “Mapato yaliyokusanywa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa yalifikia sh. bilioni 654.1 ikiwa ni asilimia 96.4 ya lengo
la kukusanya shilingi bilioni 678.8,” amesema Waziri Mkuu.
Amewataka wafanyabiashara wote wahakikishe wanatoa risiti
halali za kielektroniki za mauzo ya bidhaa na huduma wanazotoa. “Vilevile,
niwakumbushe wananchi wote kudai risiti halali za kieletroniki kila wanapofanya
ununuzi wa bidhaa na huduma ili kudhibiti upotevu wa mapato na hivyo kuimarisha
uwezo wa Serikali katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi ikiwemo maji,
elimu na afya.”
Amesema katika mwaka 2024/2025, Serikali itaendelea kuweka
vipaumbele zaidi kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi
wa bajeti kwa kuimarisha na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini
ikiwa ni pamoja na kuwianisha, kufuta au kupunguza viwango vya kodi, tozo na
ada zinazoonekana kuwa kero.
Pia itaboresha mazingira ya ulipaji kodi na kuongeza wigo wa
kodi; kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi; na kuimarisha na kuhimiza
matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA ya ukusanyaji wa mapato. “Hatua hizi
zitawezesha kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kukuza mapato ya ndani
kufikia asilimia 15.7 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na matarajio ya asilimia
15.3 mwaka 2023/2024,” amesema.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema kati ya Julai, 2023 na
Februari 2024, miradi 416 ilisajiliwa kwenye Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)
kupitia mifumo ya kusajili miradi. Amesema miradi ya Watanzania ni 153, wageni
ni 175 na ubia ni 88, sawa na ongezeko la asilimia 205 ikilinganishwa na
kipindi kama hicho mwaka 2022/2023 ambapo jumla ya miradi 203 ilisajiliwa.
“Miradi hiyo inatarajia kuwekeza jumla ya dola za Marekani
milioni 4,490 na kuzalisha ajira 119,717. Uwekezaji huo utaimarisha uchumi wa
Taifa pamoja na kuboresha maisha ya watu kupitia fursa za ajira, ukusanyaji wa
mapato na kunufaika na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii,” amesema.
Katika kipindi cha mwaka 2024/2025, Serikali itaendelea
kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuhamasisha ushiriki wa Halmashauri na
Serikali za Mikoa, sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika uendelezaji wa
maeneo ya uwekezaji na uendelezaji wa miundombinu ili kuvutia uwekezaji; na
kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wawekezaji katika ngazi zote kwa kuanzisha
benki ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji na kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji
mahususi.
Kwa mwaka 2024/2025, Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe
sh. 350,988,412,000/- ambapo kati ya fedha hizo, sh. 146,393,990,000/- ni kwa ajili
ya matumizi ya kawaida na sh. 204,594,422,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya
maendeleo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake.
Pia ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya sh.
181,805,233,000/- kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo sh. 172,124,423,000/- ni
za matumizi ya kawaida na sh. 9,680,810,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya
maendeleo.
0 Maoni