Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka wazazi kuhakikisha wanawaruhusu watoto wao wa kike wenye umri wa kuanzia miaka 9 hadi 14 kupata chanjo ya kansa ya mlango wa kizazi HPV (Human Papiloma Virus) na kusema chanjo hiyo ni salama kutokana na kufanyiwa majaribio kadhaa na wataalamu wa wizara ya afya pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Waziri Ummy ameyasema hayo Jjijini Mwanza wakati akizindua kitaifa chanjo hiyo ya kansa ya mlango wa kizazi HPV (Human Papilloma Virus) kwa watoto wa umri kuanzia miaka 9-14 na kusema chanjo hiyo ni salama na ni moja tu kwa maisha ya msichana, na kuwasihi wazazi kuwaruhusu watoto wao kuchanjwa ili kuwakinga na virusi vya ugonjwa wa kansa ya mlango wa kizazi.
"Chanjo hii huokoa maisha, huwezesha Taifa kuwa na nguvu kazi imara hivyo wazazi wote wenye watoto kuanzia miaka 9 hadi 14 nawaomba muwaruhusu kupata chanjo ni salama kabisa," alisema Mhe. Ummy.
Ameongeza kuwa virusi vya ugonjwa wa kansa ya mlango wa kizazi vinapatikana kwa wanaume na vinaweza kuingia kwa wasichana kupitia tendo la kujamiiana hivyo njia moja wapo ya kuepukana nayo ni kuacha kabisa kujihusisha na ngono katika umri mdogo.
"Tuwachanje mabinti zetu ili wasijeugua kansa ya mlango wa kizazi kwani ni hatari na pia matibabu yake ni gharama kubwa, tunasema hakuna saratani ya mlango wa kizazi Mwanza naTanzania kwa kuwapatia chanjo hii."
Katika hatua nyingine Waziri wa afya Ummy Mwalimu amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa anayoendelea kuyafanya katika sekta ya afya kwa kuongeza vituo vya kutolea huduma na vifaa tiba.
Kwa Manispaa ya Ilemela takribani watoto 40,396 wanatarajiwa kupata chanjo hiyo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa shule zote za msingi na sekondari kwa mabinti wenye umri wa miaka 9 hadi 14 kuanzia tarehe 22 hadi 28 Aprili,2024.


0 Maoni