WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amewataka wamiliki wa shule na madereva wa mabasi yanayotoa huduma za
usafiri kwa wanafunzi wajiridhishe kuhusu njia wanazopita ili kuhakikisha
kunakuwepo na usalama wa wanafunzi wanaowabeba katika vyombo vya usafiri.
“Wazazi, Walezi na Jamii ya Watanzania kwa ujumla tushiriki
kikamilifu katika kuhakikisha usalama wa wanafunzi wanapokwenda na kurudi
Shuleni wakati wote hususan katika kipindi cha mvua.”
Kadhalika amesema kwa kuwa Serikali imetoa maelekezo ya
kufunga shule zilizoathiriwa na mafuriko, halmashauri na wamiliki wa shule
zisizo za Serikali waweke utaratibu wa kufidia muda wa vipindi ili kukamilisha
kalenda ya muhula kama ilivyopangwa.
Ametoa wito huo leo (Alhamisi, Aprili 25, 2024) wakati
akitoa taarifa ya serikali kuhusu changamoto
za hali ya hewa bungeni jijini Dodoma.
Pia, amezitaka Taasisi za Serikali ziendelee, kukabiliana na
maafa kwa kushirikiana na wadau kutekeleza majukumu yaliyoanishwa katika Mpango
wa Kujiandaa na Kukabiliana na Madhara ya El-Nino pamoja na mipango ya kisekta
ili kuzuia na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
“Kamati za Maafa za Wilaya na Mikoa ziendelee kuchukua hatua
stahiki ikiwemo kutoa tahadhari kwa wananchi na kusaidia wananchi kwa wakati
pindi maafa yanapojitokeza.”
Aidha, amewataka Wakuu wa mikoa na wilaya, maafisa tarafa,
watendaji kata, mitaa na vijiji wasimamie ipasavyo usafi katika maeneo yao na
kudhibiti utupaji taka ovyo unaosababisha kuziba kwa mitaro badala ya kusubiri
usafi unaofanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
“Kwa kuwa uharibifu wa mazingira umekuwa na athari kubwa
kutokana na mabadiliko ya tabianchi, viongozi wa ngazi zote washirikiane na
wananchi kudhibiti uharibifu wa mazingira katika maeneo yao.”
Mheshimiwa Majaliwa pia amelitaka Jeshi la Polisi kupitia
Kikosi cha Usalama Barabarani liendelee kutoa tahadhari kwa madereva na
watumiaji wengine wa barabara wakati wa mvua;
“Kamati za Maafa katika ngazi za Vijiji, Wilaya na Mikoa
zisimamie kikamilifu ugawaji wa misaada inayotolewa kwa waathirika wa mafuriko
na kuhakikisha kuwa misaada inawafikia walengwa”.
Kadhalika amewataka Viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya
Vijiji wahamasishe na kuelimisha wananchi wanaoishi mabondeni kuhamia maeneo
salama ili kuepusha maafa wakati wa mafuriko na kuhakikisha wanatenga maeneo
salama yatakayotumika na wananchi watakaohamia kutoka mabondeni.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amesema kutokana
na maafa yaliyotokea nchini, Serikali kupitia Kamati za Usimamizi wa Maafa na
wadau imechukua hatua mbalimbali kwa ajili ya kuzuia, kukabiliana na kurejesha
hali.
“Hatua hizo zinajumuisha utoaji wa elimu kwa jamii ya
kujikinga na kuchukua tahadhari, kukabiliana na maafa na kurejesha miundombinu
iliyoharibika. Aidha, Serikali imetoa misaada ya kibinadamu ikiwemo chakula,
vifaa vya ujenzi, vifaa vya malazi na vifaa vya usafi.”
Amesema, hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa na misaada kutoka Serikalini na wadau kama vile uokoaji, vyakula, mahema, madawa, marekebisho ya miundombinu ya utoaji huduma imeendelea kutolewa.
“Serikali imejipanga kikamilifu na inaendelea kuchukua hatua
stahiki ili kuzuia na kupunguza makali ya majanga sambamba na kurejesha hali
katika maeneo mbalimbali yaliyoathirika.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita
imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya hali ya hewa nchini ikiwemo kufunga
miundombinu ya kisasa ya hali hewa, mafunzo kwa watumishi kwa kuzingatia vigezo
vya kitaifa na kimataifa, na kuweka mifumo wezeshi ya usambazaji wa taarifa ya
hali ya hewa pamoja na kuimarisha mifumo ya uhakiki wa ubora wa huduma.
Amesema uwekezaji wa miundombinu uliofanyika unajumuisha
ununuzi wa Rada za Hali ya hewa ambapo Rada mbili zinakamilishwa kufungwa
katika mikoa ya Kigoma na Mbeya. Vilevile, Rada nyingine mbili zinatarajiwa
kufungwa Mikoa ya Dodoma na Kilimanjaro ifikapo mwishoni mwa mwaka 2024.
“Nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwekezaji mkubwa alioufanya katika sekta ya hali ya hewa na kuijengea uwezo nchi yetu na kuifanya kuwa kinara Afrika na nje ya Afrika katika masuala ya utabiri wa hali ya hewa.”
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni