WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wote, Bara
na Visiwani waendelee kuulinda, kuuenzi, kujivunia na kuuthamini Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar.
“Kwa heshima na taadhima nitumie fursa hii kuwapongeza sana
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mheshimiwa Dkt. Hussein
Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa uongozi wao
makini ambao umekuwa chachu ya kudumisha muungano wetu.”
Ameyasema hayo jana Aprili 8, 2024) wakati akizindua nembo na
kaulimbiu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano. “Muungano huu ni tunu adimu
na adhimu inayopaswa kulindwa kwa gharama yoyote. Hivyo basi kila mmoja awe
mlinzi.”
Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano yamebeba kaulimbiu
isemayo, “Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,’ Tumeshikamana na
Tumeimarika, kwa Maendeleo ya Taifa Letu.”
Amesema Watanzania wana kila sababu ya kujivunia muungano wao
kutimiza miaka 60. “Ni ukweli usiopingika kwamba muungano wetu umeendelea kuwa
na tija kubwa na kuchagiza maendeleo ya nchi yetu na wananchi wote kwa ujumla.“
“Kama ulivyo msemo wa Kiswahili Umoja ni nguvu utengano ni
udhaifu, muungano wetu umefanya Tanzania liwe Taifa lenye utulivu, mshikamano,
nguvu na mfano kwa mataifa mengi Barani Afrika na duniani kwa ujumla.”
Waziri Mkuu amesema kilele cha sherehe za muungano
kitafanyika katika Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam, hivyo ametoa wito kwa
wananchi wote wa pande mbili za muungano wajitokeze kwa wingi ili kushuhudia
maadhimisho hayo.
“Wananchi wote tumieni maadhimisho haya kutafakari tumetoka
wapi, tuko wapi na tunaelekea wapi tangu muungano uliopoasisiwa mwaka 1964.
Kaulimbiu ya maadhimisho haya ituongoze katika tafakuri hiyo ili kwa pamoja
tuendelee kuulinda na kuutetea muungano wetu.”
Ametumia fursa hiyo kuzitaka taasisi zinazotoa elimu,
ziendelee kufundisha mada kuhusu muungano wetu kuanzia elimu ya awali ili
watoto na vijana waufahamu na wawe walinzi na hatimaye wawe vinara katika
kuundeleza.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema nchi itaendesha uchaguzi wa
viongozi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024, hivyo ametoa rai kwa wapigakura wote
wahakikishe wanajiridhisha na kushiriki taratibu za kuwafanya kuwa na sifa za
kushiriki kuchagua viongozi wenye uwezo na wenye nia njema na Muungano.
Waziri Mkuu ametoa ratiba ya matukio yatakayofanyika kuwa ni
pamoja na uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano
utakaofanyika Zanzibar tarehe 14 Aprili, 2024 pamoja na uzinduzi wa Maonesho ya
Biashara ya Taasisi za Muungano. Mgeni rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt, Hussein Ali Mwinyi.
Amesema kutakuwa na Maonesho ya Muungano kwa upande wa
Tanzania Bara yatakayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Jijini Dar es
Salaam na mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa
Hemed Abdulla.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Maadhimisho haya
yataambatana na uzinduzi wa miradi ya maendeleo utakaoanza tarehe 15 Aprili na
kuendelea hadi mwisho wa Mei, 2024.
“Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango
ataliongoza Taifa katika siku maalum ya maombi na dua kwa Taifa itakayofanyika
katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma tarehe 22 Aprili, 2024. Viongozi wa Kitaifa wa Dini zote watahudhuria
katika ibada hiyo.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema wilaya zote hapa nchini
zitaandaa maombi kwa Taifa yatakayofanyika katika siku hiyo. “Nisisitize kila
Mkuu wa Wilaya aanze kufanya uratibu ili nchi yetu yote ishiriki katika maombi
na dua hizo.”
Waziri Mkuu amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan ataliongoza Taifa katika kuzindua kitabu cha Historia ya Ofisi ya Makamu
wa Rais, shughuli itakayofanyika 23 Aprili na tarehe 24 Aprili, 2024 atatunuku
Nishani za Taifa kwa watu mbalimbali, shughuli zote zitakafanyika Ikulu, Jijini
Dar es Salaam.
“Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko (Mb), Naibu Waziri Mkuu
atakuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Muungano litakalofanyika katika Viwanja
vya Tanganyika Packers, Jijini Dar es Salaam tarehe 25 Aprili, 2024.”
Waziri Mkuu amesema kuwa tarehe 26 Aprili, 2024, Mheshimiwa
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ataliongoza Taifa katika kilele cha Maadhimisho
ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano yatakayofanyika katika Uwanja wa Uhuru,
Jijini Dar es Salaam.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni