Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa
Kagera imefanikiwa kufungua mtandao wa barabara mpya wa Kilometa 826 katika
kipindi cha miaka mitatu kutokana na ongezeko la bajeti.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa TARURA mkoa wa Kagera
Mhandisi Avithi Theodory wakati akizungumzia mafanikio ya miaka mitatu ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhandisi Theodory alisema kwamba TARURA imefanikiwa kufungua
barabara hizo mpya ambazo awali zilikuwa ni changamoto kwa wananchi wa mkoa huo
kwani walikuwa wakitembea umbali mrefu kufika eneo la huduma za jamii.
“Tumeweza kuwafungulia njia ambapo awali ilikuwa ni vikwazo
kwa wananchi kwani walikuwa wakitembea
umbali mrefu hadi kufikia huduma za kijamii, mfano mtu alikuwa akitembea Km. 21
lakini kwa sasa ni Km. 9, wapo wengine walitembea Km.8 na sasa wanatembea Km.
1.6 , hivyo tumejenga barabara mpya na sasa wananchi hawapati tena shida ya
kutumia muda mrefu kufikia huduma za kijamii katika mkoa wetu”.
Aidha, alisema Mkoa wa
Kagera umetengewa bajeti ya fedha shilingi Bilioni 31 mwaka wa fedha 2023/2024
kutoka Bilioni 9 kulinganisha na miaka
ya nyuma, jambo ambalo limefanya barabara
za mkoa wa Kagera za vijijini kufunguliwa kwa kasi na kurahisisha
maendeleo ya wakazi wa mkoa wa Kagera.
“Tangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani bajeti yetu imeweza kupanda mara tatu hadi kufikia
Bilioni 31 tofauti na bajeti ya
awali na hivyo kufanya
Barabara za mkoa wa Kagera hususani
za vijijini kufunguliwa kwa Kasi na
kurahisisha maendeleo ya wakazi wa mkoa huu,” aliongeza kusema.
Hata hivyo alisema kuongezeka kwa bajeti hiyo imeweza kuongeza barabara zenye kiwango cha lami Km.
125 kulinganisha na Km. 80 za awali,
ujenzi wa makalavati 1,600 na kufanya
maeneo mengi ya vijijini kupitika
kwa urahisi na hivyo kuweza kusafirisha
mazao yao kutoka kijiji kimoja hadi kijiji kingine na kujipatia kipato.
Pia Serikali kupitia TARURA
itaendelea kuhakikisha wanakuza miji kwa kuboresha miundombinu ya
barabara ili wananchi wakiwemo wajasiriamali na wafanyabiashara waweze
kusafirisha na kuuza bidhaa zao nyakati zote katika masoko na katika kutekeleza
hilo wamefanikiwa kufunga taa za barabarani
zipatazo 240 na nyingine 140 zinaendelea kuwekwa sehemu mbalimbali
katikati ya mji.
Naye, Bi. Kudra Kagungu, mkazi wa Biharamulo alisema kuwa Serikali inapaswa kupongezwa kwa
zawadi kubwa ya kuhakikisha miradi ya barabara inatekelezwa na wananchi
wanaondokana na kero katika matumizi ya Barabara mbaya hasa za vijijini.
Alisema uboreshaji wa barabara umeweza kuwasaidia wananchi
kujikomboa na umaskini na kuimarika kwa uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja kwani
hivi sasa maeneo mengi hakuna tena adha ya usafiri na usafirishaji wa mazao
kwani sehemu nyingi ambazo walitumia kiasi cha shilingi elfu 20,000 kufuata
mzigo kwa Sasa wanatumia shilingi elfu 3,000 hadi 5,000 kwa sababu barabara
zimeimarika.
0 Maoni