Nchi wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(Southern African Development Community-SADC) zimempongeza Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake katika
usimamizi na uhifadhi wa misitu miombo hasa katika kuhama kutoka kwenye
matumizi ya nishati ya kuni na mkaa kuelekea nishati safi ifikapo mwaka 2030.
Kauli hiyo imetolewa leo Aprili 18,2024 na Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) katika Mkutano wa Kimataifa
unaohusu Misitu ya Miombo jijini Washington DC nchini Marekani.
“Kikubwa nchi zimeweza kumpongeza Rais wetu Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa namna ambavyo amekuwa akitoa maelekezo mbalimbali kwetu sisi kama
Wizara na Sekta katika kuhakikisha
kwamba misitu ya miombo inalindwa kwa
nguvu kubwa, na kwa namna ambavyo amechukua uamuzi thabiti wa kuhakikisha
kwamba inapofika mwaka 2030 zaidi ya asilimia 80 ya wananchi watakuwa
wameachana na matumizi wa kuni na mkaa na watakuwa wamejielekeza katika nishati
safi ya kupikia,” Mhe. Kairuki amesisitiza.
Amesema kuwa misitu ya miombo nchini Tanzania na katika
ukanda wa kusini imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uharibifu
wa misitu ambao unasababishwa na ukataji wa miti usiozingatia sheria, taratibu
na kanuni, moto, kilimo cha kuhamahama, uharibifu wa vyanzo vya maji na
mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha, amefafanua kuwa kupitia mkutano huo, wadau mbalimbali
wameanza kuonesha nia ya kusaidia mpango wa utekelezaji wa Azimio la Maputo la
mwaka 2022 kuhusu ulinzi na uendelezaji wa misitu ya miombo.
Amesema lengo la Mkutano huo ni kuona namna ya kuendeleza
Azimio la Maputo katika kulinda na kuendeleza Misitu ya Miombo ambapo takribani
asilimia 93 ya misitu ya Tanzania ni miombo ambayo pamoja na mambo mengine,
inatunza wanyamapori, vyanzo vya maji na huduma nyingine za kijamii.
Naye, Kamishna Uhifadhi wa Wakala ya Huduma za Misitu
Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo
amesema kuwa kupitia mkutano huo nchi za SADC zimekuwa na majadiliano
kuhusu kutafuta namna ya kushirikiana baina ya
nchi hizo na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kupata rasilimali
fedha na kukuza ujuzi na utaalamu kwa ajili ya kusaidia uhifadhi wa misitu
hiyo.
Amoengeza kuwa kongamano hilo limehitimishwa na hotuba ya
Rais wa Jamhuri ya Watu wa Msumbiji, Mhe. Filipe Nyusi ambapo amesisitiza
umuhimu wa nchi hizo kushirikiana katika kubadilishana taarifa , kukabiliana na
masuala ya uharibifu wa mifumo ya ikolojia ya miombo hususan biashara haramu za
mazao ya misitu na wanyamapori katika ukanda wa SADC.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Deusdedith Bwoyo amesema kuwa mkutano huo umekuwa ni wa kipekee na muhimu ambapo nchi 11 zimebaini kuwa umoja ni nguvu na kwamba kila nchi haiwezi kusimamia kwa ufanisi mkubwa misitu yake na hivyo, zimekutana na kujadili kwa pamoja changamoto za misitu ya miombo na namna ya kuunganisha nguvu na kutafuta rasilimali fedha katika usimamizi na uendelezaji wake kwa faida ya kizazi cha sasa na vijavyo.
0 Maoni