Baadhi ya Wazee wa kimila (Malaigwanan) kutoka ndani ya
Hifadhi ya Ngorongoro wamekata shauri na kuamua kuondoka ndani ya hifadhi hiyo
kuelekea Kijiji cha Msomera na maeneo mengine baada ya kupata elimu ya umuhimu
wa kwenda kufanya shughuli nyingine ili kuboresha maisha yao na kupisha
shughuli za uhifadhi.
Katika kikao maalum kilichofanyika jana usiku tarehe 10.04.2024 katika Kijiji cha
Meshili kata ya Olbalbal na kuhudhuriwa
na baadhi ya wazee hao wa kimila (Laigwanan) ambao wamesema kuwa wamechoka
kupotoshwa kwa kupewa fedha ndogondogo ili wasiihame katika eneo hilo.
Wameongeza kuwa
baadhi ya viongozi wa kisiasa na wanaharakati wa tarafa ya Ngorongoro wamekuwa
wakitoa fedha kwao ili waendelee kubaki na umaskini wakati viongozi wakubwa
wanaowashawishi wasihame wengi wao wanaishi mjini Karatu na Arusha huku wao
wakiishi katika maisha magumu na wengine kupoteza familia zao kwa kuliwa na
wanyama.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao malaigwanan hao wamesisitiza kuwa kwa sasa
wamejipanga kuondoka na tayari wapo kwenye kufuata taratibu za uandikishaji ili
waweze kutoka kwenye eneo hilo na kuelekea katika Kijiji cha Msomera na maeneo
mengine.
“Tumechoka kudanganywa na watu ambao wamekuwa wakiishi kwa
kupata fedha kutoka kwa wanasiasa na wadau wengine kupitia migongo
yetu,wanatudanganya tusihame wakati wao wenyewe hawakai humu hifadhini,viongozi
wetu ni wababaishaji na hawatujali zaidi ya kuendekeza matumbo yao”alisema kiongozi mmoja wa wazee hao wa kimila.
Wameongeza kuwa baadhi ya watoto wa tarafa hiyo wamegeuzwa
kuwa wachungaji wa mifugo ya matajari kutokana na umaskini wa familia zao ndio
maana ni kawaida hata siku za shule kukuta watoto hao wakiwa machungani badala
ya kuwa shule.
Katika siku za hivi karibuni uchunguzi wa mwandishi wetu
unaonesha kwamba kumekuwa na vikao vya mara kwa mara vya viongozi wa kimila
ndani ya tarafa ya Ngorongoro kujadili mustakabali wao baada ya idadi kubwa ya
waandishi kushawishika kuhama kutoka ndani ya hifadhi.
Viongozi hao wa kimila wamekuwa wakiziomba mamlaka
zinazohusika na zoezi hilo kuwahamisha haraka kutoka ndani ya hifadhi baada ya
kupata taarifa za jinsi wenzao wanavyoishi maisha mazuri, salama na yenye uhuru
mkubwa katika Kijiji cha Msomera kulinganisha na maisha ndani ya hifadhi.
Na. Mwansishi Wetu- Ngorongoro
0 Maoni