WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetumia sh.
trilioni 10.69 kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa
yenye urefu wa kilometa 1,219 kuanzia Dar es Saalam hadi Mwanza.
Akielezea utekelezaji wa miradi nane ya kielelezo kwa mwaka
2023/2024 Bungeni leo (Jumatano, Aprili 3, 2024), Waziri Mkuu amesema hadi
kufikia Februari 2024, ujenzi wa reli hiyo umefikia viwango vya kati ya
asilimia 5.38 na asilimia 98.84, tayari reli hiyo imeshaanza kufanyiwa
majaribio kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro.
“Kama nyote mlivyoshuhudia, majaribio ya treni hiyo ya mwendo
kasi yalifanyika kwa mafanikio makubwa mwezi Februari, 2024. Ni matarajio yetu
kuwa huduma ya usafiri na usafirishaji itaanza ifikapo Julai, 2024 kwa kipande
cha Dar es Salaam hadi Dodoma,” amesema Waziri Mkuu wakati akiwasilisha Taarifa
ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2023/2024 na Mwelekeo
wa Kazi zake kwa mwaka 2024/2025.
Akifafanua kuhusu ujenzi wa reli hiyo, Waziri Mkuu amesema:
“Ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam - Morogoro (52.69, Makutupora - Tabora
(Kilomita 371) umefikia asilimia 13.86, Tabora - Isaka (Kilomita 165) umefikia
asilimia 5.38 na Tabora – Kigoma (Kilomita 506) umefikia asilimia 1.81 Kilomita
300) umefikia asilimia 98.84, Morogoro – Makutupora (Kilomita 422) umefikia
asilimia 96.35, Mwanza - Isaka (Kilomita
341) umefikia asilimia.”
Akielezea kuhusu mradi wa kuzalisha umeme wa wa Julius
Nyerere ambao unatarajiwa kuzalisha megawati 2,115, Waziri Mkuu amesema
utekelezaji wake umefikia asilimia 96.81 na kwamba kazi zote za mradi huo
zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Desemba, 2024.
Amesema zoezi la kuwasha mtambo wa kuzalisha umeme
lilifanyika na kufanikiwa kuingiza kwenye Gridi ya Taifa megawati 235 kutoka
kwenye mtambo mmoja kati ya mitambo tisa itakayozalisha umeme katika mradi huo.
Kuhusu uboreshaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Waziri
Mkuu amesema Serikali imekamilisha malipo ya sh. bilioni 753 kwa ajili ya ndege
tatu aina ya Boeing 737-9 Max (ndege mbili) na Boeing 787-8 (ndege moja).
“Ndege mbili aina ya Boeing 737-9 Max ziliwasili nchini Oktoba, 2023 na Machi,
2024 na nyingine moja inategemewa kuwasili Aprili, 2024 na hivyo kulifanya
Shirika hilo liwe na jumla ya ndege 16.”
Akielezea kuhusu mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la
Afrika Mashariki kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga lenye urefu wa
km. 1,443, Waziri Mkuu amesema Serikali tayari imechangia jumla ya dola za
Marekani milioni 268.77 sawa na asilimia 87.27 ya hisa zake.
“Hadi kufikia Machi, 2024 baadhi ya shughuli zilizofanyika ni
kukamilisha ulipaji wa sh. bilioni 34.93 zikiwa ni fidia kwa wananchi 9,823 kati ya 9,904 wanaopisha
eneo la mradi; kukamilika na kuzinduliwa kwa kiwanda cha kusimika mifumo ya
kupasha joto na kuzuia upotevu wa joto kwenye bomba kilichopo Wilaya ya Nzega;
na kuanza ujenzi wa matanki manne yenye ujazo wa mapipa 500,000 kila moja ya
kuhifadhia mafuta ghafi kabla ya kupakiwa kwenye meli katika eneo la
Chongoleani, Tanga.”
Kuhusu mradi wa kiwanda cha sukari Mkulazi, Waziri Mkuu
amesema ujenzi wake umefikia asilimia 99 na umegharimu sh. bilioni 320.05 na
umetoa fursa za ajira 1,996. “Kiwanda hicho kimeanza uzalishaji tangu Desemba,
2023 na hadi kufikia Machi 2024, tani 1,851 za sukari zimezalishwa na kupelekwa
sokoni. Matarajio ya kiwanda ni kuzalisha tani 50,000 kwa mwaka ifikapo mwaka
2026/2027,” ameongeza.
Kuhusu mradi wa daraja la Kigongo - Busisi (Mwanza) lenye
urefu wa kilomita 3.2 pamoja na barabara unganishi yenye urefu wa kilomita 1.66
kwa kiwango cha lami, Waziri Mkuu amesema ujenzi wake umefikia asilimia 84.47
na unatarajiwa kukamilika Desemba, mwaka huu. Mradi huu utagharimu sh. bilioni
716.33.
Mradi mwingine ambao Waziri Mkuu ameuelezea ni kiwanja cha
ndege cha kimataifa cha Msalato kilichopo Dodoma ambacho ujenzi wake umefikia
asilimia 54.1 na kwamba hadi kufikia Februari, 2024 zimetumika sh. bilioni
107.64.
Amezitaja kazi zinazoendelea kuwa ni ujenzi wa barabara ya
kuruka na kutua ndege, barabara ya viungio, maegesho ya ndege pamoja na
usimikaji wa taa za usalama na kuongozea ndege. Ujenzi wa jengo la abiria na
majengo mengine utekelezaji umefikia asilimia 17.1.
Kuhusu ujenzi wa meli ya MV. Mwanza “Hapa Kazi Tu”, Waziri
Mkuu amesema umefikia asilimia 93 ambapo Serikali imetumia dola za Marekani
milioni 44.823 sawa na asilimia 90.87 ya gharama zote za mradi huu ambao
unatarajiwa kukamilika Mei, 2024. “Kukamilika kwa mradi huu kutaboresha huduma
za usafiri wa abiria na mizigo kwa njia ya meli katika mikoa ya Kanda ya Ziwa
na nchi za jirani za Kenya na Uganda, na kufungua nchi kiuchumi pamoja na kuchochea
ukuaji wa sekta ya utalii,” amesema.
Kwa mwaka 2024/2025, Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe
sh. 350,988,412,000/- ambapo kati ya fedha hizo, sh. 146,393,990,000/- ni kwa
ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 204,594,422,000/- ni kwa ajili ya matumizi
ya maendeleo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake.
Pia ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya sh.
181,805,233,000/- kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo sh. 172,124,423,000/- ni
za matumizi ya kawaida na sh. 9,680,810,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya
maendeleo.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni