WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mahakama zimeanza
kutumia mfumo unaonasa sauti na kuzibadilisha kwenda kwenye maandishi huku
ukitafsiri lugha za Kiingereza na Kiswahili.
“Hii ni hatua kubwa sana kwani mfumo huo unarekodi sauti na
kupeleka kwenye maandishi. Vilevile, unaweza kutafsiri lugha ya Kiswahili au
Kiingereza kulingana na uhitaji,” amesema na kuongeza: “Kanuni za Mahakama
zimeanza kutafsiriwa sambamba na uandaaji wa mihutasari ya hukumu kwa Kiswahili
ili kuwawezesha wananchi kuelewa mwenendo wa mashauri.”
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Aprili 15, 2024) Bungeni,
jijini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuhitimisha mjadala wa bajeti ya Ofisi ya
Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2024/2025.
Akielezea mambo yaliyofanyika ndani ya miaka mitatu ya
Serikali ya awamu ya sita, Waziri Mkuu amesema mbali ya matumizi ya Kiswahili
mahakamani, Serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA ili kuendana na
kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia kutokana na mapinduzi ya nne ya viwanda duniani.
“Jitihada hizo zimeanza kuleta mafanikio katika utendaji wa
Serikali kwa kuunganisha Serikali yote (Wizara, Idara, Wakala na Taasisi zake)
ziweze kusomana kimfumo. Tumeanza kupata mafanikio mfano: Mahakama ya Tanzania,
ambapo mifumo mbalimbali ya TEHAMA imejengwa ili kurahisisha na kuharakisha
utoaji wa haki kwa wananchi.”
Waziri Mkuu ameitaja mifumo hiyo kuwa ni pamoja na Mfumo wa Usajili, Uendeshaji na Usimamizi wa
Mashauri kwa ajili ya kurahisisha, kuharakisha na kuokoa muda wa mwenendo wa
mashauri mahakamani.
“Mfumo mwingine ni wa unukuzi na kutafsiri mienendo ya
mashauri Mahakamani kwa lengo la kuwa suluhu ya kudumu ili kuwawezesha
Waheshimiwa Majaji na Mahakimu kuondokana na adha ya kuandika kwa mkono
mwenendo wa mashauri,” ameongeza.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema katika kuhakikisha mfumo
wa utoaji haki unaboreshwa, Januari 31, 2023, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
aliunda Tume maalum aliyoipa jukumu la kushauri namna njema ya kuboresha mfumo
na utendaji kazi wa taasisi zinazohusika na haki jinai.
Akielezea maboresho ya mfumo wa utoaji haki na taasisi za
hakijinai, Waziri Mkuu amesema: “Tume hiyo, ilipokea maoni kutoka kwa wananchi
na wadau wengine wa hakijinai na kutoa mapendekezo ya maboresho yanayohitajika
kufanyika. Tangu Tume ilipowasilisha mapendekezo, Serikali imekuwa ikichukua
hatua mbalimbali za maboresho ya mfumo wa utoaji wa hakijinai ikiwemo kuboresha
mazingira ya kufanyia kazi kwa taasisi za hakijinai.”
Amesema Serikali inaendelea kufanyia kazi mapendekezo yote
yaliyotolewa ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata haki zao kwa wakati na
waweze kuendelea kufanya shughuli za maendeleo yao binafsi na Taifa zima kwa
ujumla.
“Hii ndiyo dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan ya kukidhi kiu na matarajio ya wananchi ya utoaji wa hakijinai kuanzia
hatua za uchunguzi, ukamataji wa watuhumiwa hadi utoaji wa hukumu yenye haki
mahakamani,” amesisitiza.
Kwa mwaka 2024/2025, Bunge limeidhinisha sh.
350,988,412,000/- ambapo kati ya fedha hizo, sh. 146,393,990,000/- ni kwa ajili
ya matumizi ya kawaida na sh. 204,594,422,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya
maendeleo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake.
Vilevile, Bunge limeidhinisha sh. 181,805,233,000/- kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo sh. 172,124,423,000/- ni za matumizi ya kawaida na sh. 9,680,810,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
0 Maoni