WAZIRI MKUU Kasim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu
wa Wilaya waweke utaratibu wa kutoa taarifa za michango inayotolewa na wadau
kwenye maafa ili kujenga imani kwao.
“Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao ni wakuu wa
Kamati za Maafa kwenye maeneo yao watoe mrejesho ili kuweka uwazi na kujenga
imani kwa wadau juu ya matumizi ya fedha zilizotolewa.”
Ametoa wito huo Bungeni leo (Alhamisi, Aprili 18, 2024)
wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Agnes Hokororo kwenye kipindi
cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
Mbunge huyo alitaka kujua Serikali ina mkakati gani wa
kuhakikisha inasimamia michango inayotolewa na inatoa mrejesho wa fedha
zinazochangwa na wadau mbalimbali ili kukarabati majengo ya umma yaliyoharibiwa
pindi majanga yanapotokea.
Waziri Mkuu amesema kwenye maeneo yoyote yanayokumbwa na
maafa kama vile moto au mafuriko, zipo kamati maalum za maafa kuanzia ngazi za
Kijiji, Kata, Wilaya na Mkoa ambazo zina wajibu wa kuratibu masuala yote
ikiwemo misaada inayotolewa katika maeneo yao. “Kamati hizi kwa ngazi za wilaya
na mkoa huongozwa na Wakuu wa Wilaya na Mikoa wa maeneo husika. Hivyo wanao
wajibu wa kutoa taarifa juu ya matumizi ya michango inayotolewa na wadau,”
amesisitiza.
Akitoa mfano juu ya suala hilo, Waziri Mkuu aliyataja
majanga ya kuungua moto soko la Moshi na Shule ya Sekondari Lindi kama baadhi
ya maeneo ambayo yanatakiwa kutolewa taarifa za michango ya wadau ili wajue
matumizi ya fedha zao.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kusimamia kilimo na kuhamasisha
wakulima wa mazao yote ya biashara na chakula ili waweze kulima kwa urahisi
zaidi na kupata huduma kwa gharama nafuu.
“Sasa hivi tunatoa huduma hizo kwenye mbolea, dawa na zana
za kilimo…, tumepunguza kodi kwenye vifaa vyote vya kilimo na hii ndiyo ruzuku
ambayo tunaizungumzia. Tunapotoa ruzuku ya mbolea, mkulima anaweza kuitumia
kwenye mazao yote,” amesema wakati akijibu swali la Dkt. Christine Mnzava (Viti
Maalum) aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kutoa ruzuku kwa mazao yote
ya biashara ikiwemo zao la pamba.
Ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ruzuku ya sh. bilioni 50
kila mwaka kwa miaka miwili mfululizo ili zitumike kuagiza pembejeo ambazo
zimesadia kuongeza uzalishaji wa mazao. “Mwaka wa kwanza alitoa shilingi
bilioni 50 na mwaka jana akatoa tena shilingi bilioni 50 ambazo tumenunua
mbolea na dawa za kilimo na kutoa ahueni kwa wakulima wa Tanzania.”
Mapema, Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kupokea
maoni na kufanya mapitio ya sheria zilizopo kuhusiana na masuala ya ukatili wa
kijinsia ili jamii ibaki kuwa salama.
“Inawezekana makosa haya yanajirudia kwa sababu baadhi ya
maeneo yana sheria lakini sheria zake si kali sana; na jambo hili ni mtambuka
na linagusa wizara nyingi na kila wizara inaweka sheria zake katika kukinga
jambo hili. Napokea ushauri wa kufanya mapitio kwani tunatamani kuona jambo
hili likikoma kwenye jamii yetu.”
“Niiase jamii yetu izingatie mila, desturi na tamaduni zetu
ili tusiingie kwenye matendo haya ya unyanyasaji wa kijinsia kwa sababu kila
mmoja na haki ya kuishi; kupunguza ulevi holela na kuacha imani potofu za
baadhi ya makabila.”
Alikuwa akijibu swali la Tunza Malapo (Viti Maalum) ambaye alisema Serikali haioni kuwa kuna haja ya kuangalia upya sheria zilizopo ama kuongeza adhabu ili kukabiliana na matukio ya unyanyasaji wa kijinsia ambayo yanazidi kushika kasi katika jamii.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni