Mkuu wa Wilaya ya Handeni mheshimiwa Wakili Albert Msando
amesema serikali haitoruhusu mtu yeyote kufanya vitendo vya utapeli na
udanganyifu katika zoezi la kuhamisha wananchi kwa hiyari kutoka ndani ya
hifadhi ya Ngorongoro kwenda katika Kijiji cha Msomera kilichopo Wilaya ya
Handeni mkoani Tanga.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Kijiji cha Msomera
Handeni tarehe 11 Aprili, 2024 Wakili Msando
amesema amefika katika Kijiji hicho ili kukutana na mwananchi yeyote ambaye
anaamini kuwa serikali haijamtendea haki wakati wa kuhama kutoka ndani ya
hifadhi kwenda kijijini hapo ili aweze kusikilizwa na kutatua changamoto yoyote
kuhusiana na madai hayo.
Wakili Msando amesema kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya
wananchi ambao wakati wanahama kutoka Ngorongoro kwenda kijijini hapo walikuwa
wategemezi katika kaya mbalimbali ambazo zililipwa stahiki zao zote za
maendelezo ya mali zao pamoja na motisha ambao wamejitokeza na kudai kuwa
wametapeliwa na serikali kitu ambacho si cha kweli.
"Wananchi 132 ambao waliorodhesha majina yao na
kuyaleta kwangu niliyatuma majina hayo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na
serikali imegundua kuwa watu hao hawakuwa wakuu wa kaya wakati wanahama, Kuna
watu wanataka kuleta utapeli katika zoezi hili na wengine wapo nchi za nje
wakiamini kwamba kuna fedha za bure ili wafanye utapeli hilo halikubaliki na
ndio maana leo nimekuja tena hapa niwasikilize kama wana jambo lolote la ziada,”
alisema Mh.Msando.
Kuhusu wananchi watatu ambao majina yao yameongezeka katika
taarifa iliyotolewa na baadhi ya vyombo vya habari jana Mhe.Msando amesema vyombo husika
vinafuatilia madai yao kuona kama yana ukweli na kuuhakikishia umma kwamba
hakuna mwananchi yeyote ambaye atakubali kuhama kwa hiyari asipate haki zake anazostahili
kwa mujibu wa sheria.
Mkuu huyo wa Wilaya mesisitiza kuwa zoezi la kuhamisha watu
kutoka ndani ya hifadhi ni la hiyari na ndiyo maana wahusika wote wanahusishwa
kuanzia hatua ya uelimishaji, uandikishaji, uthaminishaji na uhamishaji wa
wananchi na mali zao ambapo kila mwananchi anayekubali kuhama husaini fomu
mbalimbali zinazomuwezesha kupata stahiki zake kwa haraka.
Mhe. Msando ametoa wito kwa wananchi wanaokubali kuhama kwa
hiyari kutumia fedha wanazozipata kufanya maendelezo katika maeneo wanayopewa na serikali badala ya
kutumia fedha hizo kwa mambo mengine na mwisho wa siku kutoa lawama kwa
serikali na kuanzisha madai mengine.
Vilevile amewataka waandishi wa habari wote wanaotaka kufahamu
ukweli baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi kuwasiliana na mamlaka
zinazohusika badala ya kuupotosha umma kwa taarifa zisizo na ukweli wowote kwa
kuegemea upande mmoja.
Jumla ya wananchi 132 ambao ni wategemezi wa kaya zilizohama kwa hiyari kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kwenda katika Kijiji cha Msomera waliripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari wakidai kwamba serikali haijawapa stahiki zao wakati wa zoezi hilo la kuhama kitu ambacho kilikanushwa pia na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Na. Mwandishi Wetu- Handeni
0 Maoni