Fisi aua watoto watatu wa familia moja

 

Mnyama Fisi amewang’ata na kuwaua watoto watatu wa familia moja katika Kata ya Kambikatoto, Tarafa ya Kipembawe, wilayani Chunya katika Mkoani Mbeya.

Polisi mkoani Mbeya wamesema hii leo kuwa fisi huyo alivamia jana katika nyumba ya Shigela Ngasa (45) Mkazi wa Gengeni na kuwang’ata watoto Samweli Shigela (5), Kasunzu Shigela (03) na Ngasa Shigela mwaka 1.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mbeya, SACP Abdi Issango, amesema mnyama huyo pia aliwajeruhi wazazi wa watoto hao ambaoni Shigela Ngasa [baba] na mke wake aitwaye Limi Masanja (38) wote wakazi wa Gengeni.

Kamanda Issango amesema baada ya tukio hilo Fisi huyo aliua kondoo wawili na kisha akakimbia uelekeo wa Hifadhi ya Rungwa eneo la Kambikatoto.

Amesema Fisi huyo aliweza kuingia ndani ya nyumba hiyo kutokana na nyumba hiyo kutokuwa na mlango na ipo porini karibuna Hifadhi hiyo.

Kamanda huyo amesema majeruhi wamelazwa Hospitali ya Mtakatifu Gasper- Itigi, Wilaya ya Manyoni, Mkoa wa Singida kwa matibabu zaidi.

Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Askari wa wanyamapori kutoka Pori la Akiba la Rungwa na wananchi wa Gengeni limefanikiwa kumuua Fisi huyo ambaye alikimbilia Porini na baadae kurudi tena Kijijini hapo.

Chapisha Maoni

0 Maoni