Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan
Abbasi, leo Aprili 8, 2024, amefungua Semina Elekezi kwa watumishi wa ajira
mpya 96 waliohitimu mafunzo ya awali ya Uhifadhi na kuwa tayari kuanza majukumu
yao kama watumishi wa umma.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania (TFS) na kufanyika katika Chuo cha Viwanda na Misitu (FITI) mjini
Moshi yanalenga kuwaandaa vijana hao kuanza majukumu yao ya Utumishi wa Umma
wakiwa na maadili na kuijua misingi ya utumishi wao.
Akizungumza katika ufunguzi huo Dkt. Abbasi amewaasa
kuzingatia maadili watakapokuwa kazini, kufanya kazi kwa bidii na kujiwekea
malengo makubwa.
“Pamoja na mambo mengine niliyowaeleza yatakayowasaidia
kufika mbali suala la maadili ndio msingi mkuu. Mnakwenda kuwahudumia wananchi
katika maeneo mbalimbali ya misitu nchini ni matarajio yetu mtawahudumia
wananchi na pale wanapokosea kuwaelimisha badala ya kutumia nguvu au kupokea
rushwa kuacha raslimali zikiharibiwa. Binafsi nikisikia hayo kwenu nitasikitika
sana na tutachukua hatua kali,” alisema Dkt. Abbasi.
Akiwa Chuoni hapo pia ametembelea Chuo cha Viwanda na Misitu
(FITI) na kuzungumza na wafanyakazi ambapo amewaeleza kuwa Serikali ya Awamu ya
Sita inakijali mno Chuo hicho na mipango ya kukiboresha imeanza ikiwemo
kuongezewa bajeti kwa zaidi ya asilimia 100 katika mwaka wa fedha utakaoanza
Julai, 2024.
Watumishi wa ajira mpya 96 waliohitimu mafunzo ya awali ya Uhifadhi na kuwa tayari kuanza majukumu yao kama watumishi wa umma, wakimsikiliza kwa maakini Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, leo Aprili 8, 2024.
Na Mwandishi Wetu- Moshi
0 Maoni