Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk.
Emmanuel John Nchimbi, amesema kazi kubwa iliyofanywa na Serikali, chini ya
uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan, ndani ya miaka mitatu, ni nyezo
inayobeba ukweli wa kutosha kusambaratisha uongo unaoenezwa na baadhi ya
wapinzani wa kisiasa kupitia mikusanyiko yao.
Amewataka wana-CCM wote kuendelea kujiamini na kutembea
kifua mbele wanapozisema, kuzitangaza na kuikumbusha jamii kuhusu kazi za
maendeleo na ustawi wa jamii, zinazofanywa na Serikali za CCM ili wananchi
waendelee kuuona ukweli, wakitofautisha na uongo unaoenezwa kwa propaganda
nyepesi za kisiasa.
Balozi Dk. Nchimbi amesema hayo leo, Aprili 19, 2024,
alipokuwa akiwahutubia maelfu ya wanaCCM wa Mkoa wa Njombe, kupitia Mkutano
Maalum wa Mkoa, uliofanyika mjini
Njombe.
“Mambo yaliyofanywa na Serikali ndani ya hii miaka mitatu,
unaweza kuona kama ni miujiza. Kazi kubwa sana inafanyika. Ni wajibu wetu
kuitumia nyenzo yenye ukweli kupambana,” amesema Balozi Dk. Nchimbi.
Kupitia mkutano huo, ambao Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka aliwasilisha taarifa ya mrejesho wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020 - 2025, iliyohusisha miradi mbalimbali ya maendeleo na ustawi wa wananchi, Balozi Nchimbi pia amerudia kusisitiza kwa watendaji wa Chama na Serikali ulazima na umuhimu wa kuwa waadilifu wakati wote kwenye masuala yanayohusu rasilimali za umma, kwa kupiga vita rushwa na ubadhirifu.
0 Maoni