TFF yajitenga na kauli ya Waziri Dkt. Ndumbaro

 

Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limejitenga na kauli iliyotolewa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro, kuhusiana na kutumika pasipoti ya Afrika Kusini kwa mashabiki watakao vaa jezi za Mamelodi Sundowns kwenye mechi dhidi ya Yanga.

Waziri Dkt. Ndumbaro alitoa kauli hiyo hivi karibuni, katika kile anachoamini kuwa ni kuhamasisha uzalendo wa kuzishangilia timu za nyumbani katika michuano ya kimataifa na kuachana na siasa za ushabiki wa Simba na Yanga.

Katika barua yao waliyoituma kwa Mkuu wa Ulinzi na Usalama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), TFF wameihakikishia CAF kuwa mchezo huo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika utafanyika kwa kuzingatia kanuni zilizopo na taratibu za kuingia uwanjani.

“Hakutatumika pasipoti kwa mashabiki wa Mamelodi Sundowns ili kuingia katika dimba la Mkapa, na kwa vyovyote vile mechi za mpira wa miguu hazisimamiwi na Idara ya Uhamiaji,” imesema barua hiyo iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred.

Barua hiyo imesema timu ya Mamelodi Sundowns maafisa wake na mashabiki wanahakikishia ulinzi wawapo nchini kwa michezo wao dhidi ya Yanga, na hata mashabiki wao wanaoishi Tanzania wataruhusiwa kuingia dimbani kushuhudia mchezo huo.

Yanga imepangiwa kukutana na Mamelodi Sundowns katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo itashuka katika dimba la Mkapa Jijini Dar es Salaam katika mchezo wao wa wali Jumamosi Machi 30, 2024.



Chapisha Maoni

0 Maoni