Nchi Wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC) zimetakiwa kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa nchi zao
zinakuwa na amani, umoja na utulivu na kutafuta ufumbuzi wa migogoro kwa kutumia
njia zao wenyewe.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Mkutano wa Dharura wa Kamati
ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambaye pia ni Kaimu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mhe. Mulambo
Haimbe wakati anafungua Mkutano huo uliofanyika jijini Lusaka, Zambia Machi 22,
2024.
Tanzania inatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi hiyo baada ya
Zambia na inawakilishwa katika Mkutano huo na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe January Makamba (Mb) na Waziri wa Ulinzi
na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb).
Mkutano huo pamoja na mambo mengine unapokea ripoti ya
utekelezaji wa vikosi vya kulinda amani katika Jimbo la Cabo Delgado nchini
Msumbiji na mchakato unaoendelea wa kupeleka vikosi vya kulinda amani Mashariki
mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Nchi Wanachama zimehimizwa kuimarisha zaidi mshikamano na
kuchangia rasilimali walizonazo ili kuviangamiza vikundi vya waasi
vinavyotishia amani kwenye Kanda ya SADC. Imeelezwa kuwa bila ya amani na
Usalama katika Kanda hiyo, wananchi wasitarajie kufikiwa kwa mtangamano na
maendeleo ya kweli.
Mkutano huo wa Mawaziri ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa
Nchi na Serikali wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya SADC utakaofanyika Machi
23, 2024 ambapo Tanzania itawakilishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.


0 Maoni