TAWIRI yatambulisha zao la asali ya masega

 

Taasisi  ya  Utafiti  wa  Wanyamapori  Tanzania ( TAWIRI)  ni miongoni mwa taasisi  zilizopo chini ya Wizara  ya Maliasili  na Utalii zinazoshiriki maonyesho siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji Miti Kitaifa inayoadhimishwa leo 21, Machi 2024.

Akizungumza katika maonesho hayo yanayoendelea Wilayani Same- Kilimanjaro, Mtafiti kutoka TAWIRI,  Kipemba  Ntiniwa  amewakaribisha wananchi kutembelea banda la TAWIRI  kujifunza na kupata ushauri wa tafiti za Wanyamapori na makazi yao ikiwa ni pamoja na Misitu, ufugaji bora wa Nyuki na uongezaji thamani mazao ya Nyuki.

Ntiniwa ameeleza tofauti na mazao ya nyuki yaliyozoeleka,  kwa sasa TAWIRI  imeandaa zao jipya la Asali ya MASEGA ya Nyuki wakubwa ( COMB  HONEY ) ambayo ni muhimu kwa afya ya Binadamu kwani inasaidia kupunguza “cholesterol” kwenye damu, kuimarisha kinga za mwili (antioxidant, antifungal na antibacterial), kusaidia mmeng'enyo wa chakula na kuimarisha msukumo wa damu.

 "Asali ya Masega ina vitamini C, B6, B12, A, E,D na haijafanyiwa uchakataji, haijayeyushwa, haijachachishwa  ipo katika hali yake ya uhalisia kama ilivyotengenezwa  na Nyuki kwenye masega ndani ya Mzinga, " ameeleza Ntiniwa.

Aidha, Ntiniwa  ametoa wito kwa jamii kutunza Misitu kwani inaumuhimu mkubwa kwa viumbe  hai akiwemo  Binadamu, ambapo amebainisha  katika uhifadhi misitu ni makazi ya  Wanyamapori akiwemo Nyuki, Ndege na Wadudu.Pia Miti na mimea mbalimba iliopo katika Misitu ni chakula cha Wanyamapori. Pia misitu inahifadhi maji na ni maeneo ya mazalia ya viumbe mbalimbali.

Ikumbukwe, Misitu ni muhimu sana katika udhibiti wa madhara ya mabadiliko ya tabia ya nchi.



Chapisha Maoni

0 Maoni