Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Rais Samia Suluhu Hassan
ni kinara na kielelezo cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoigusa jamii
ya Watanzania.
Amesema kuwa maono na misingi iliyojengwa na Rais, Dkt. Samia
imewezesha Serikali ya awamu ya sita kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo
ikiwemo miradi ya kimkakati na kuimarisha utoaji wa huduma za jamii.
"Serikali imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya
usafiri na usafirishaji kwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya
kuimarisha usafiri wa anga, usafirishaji kwa njia ya reli, barabara na usafiri
katika bahari na maziwa makuu."
Amesema hayo leo (Jumamosi, Machi 30, 2024) wakati wa Kongamano
wa Maadhimisho ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia lililofanyika Mkoani Mwanza.
Aidha, amesema kuwa
katika utekelezaji wa miradi ya usafiri katika maziwa makuu Serikalk imeendelea
kutekeleza mradi wa ujenzi wa meli ya Mv. Mwanza Hapa Kazi Tu yenye uwezo wa
kubeba abiria 1200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20 na malori matatu na
hadi sasa umefikia asilimia 94 ya ujenzi wake.
Amesema sambamba na ujenzi wa meli katika maeneo mbalimbali,
Serikali pia imefanya maboresho katika bandari na kuongeza ufanisi wa utoaji
huduma katika bandari hizo ikiwemo bandari kwenye Ziwa Victoria.
Ameongeza kuwa katika
kuimarisha Sekta ya kilimo, Serikali imeendelea kuboresha usimamizi na utoaji
wa huduma kwa kuongeza Bajeti katika
Wizara ya Kilimo.
"Serikali imeweka msisitizo katika usimamizi wa zao la
Pamba ikiwemo kuongeza thamani ya zao hili nitoe wito kwa wakulima wa zao hili
kuongeza uzalishaji ili mahitaji tuliyonayo yaendane na uhitaji uliopo."
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea na
ujenzi wa mradi wa Bandari ya Uvuvi pamoja na kutoa zana bora, pembejeo na
vifaa muhimu vitakavyowawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi lengo ni
kuhakikisha sekta hiyo inachangia Pato la Taifa na uchumi wa mtu mmoja mmoja.
"Katika kuimarisha Sekta ya uvuvi Rais amewezesha
kununuliwa na kusambaza boti 160 za kisasa za uvuvi zenye thamani ya shilingi
bilioni 11.5 kwa vyama vya ushirika wa wavuvi, watu binafsi na vikundi vya
wavuvi katika Halmashauri 58."
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa
Wafanyabiashara wa Tanzania kutumia fursa za uwekezaji zilizowekwa na Serikali
ya awamu ya sita ili kukuza uchumi wa Nchi na uchumi wao binafsi.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana ambaye alimwakilisha Mkuu
wa Mkoa huo amesema Serikali imefanya kazi kubwa katika kuboresha Sekta ya
elimu, afya na miundombinu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Jukwaa la Mafiga Matatu, Aloyce Nyanda amesema kongamano hilo ni
sehemu ya kutambua mchango mkubwa wa miradi uliyotekelezwa na Rais Samia Suluhu
Hassan kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Tanzania nzima kwa ujumla.
Kongamano hilo limehudhuriwa na watu wa kada mbalimbali
ikiwemo wabunge, wahadhiri, watumishi wa Serikali, wafanyabiashara na wanafunzi
wa vyuo mbalimbali jijini Mwanza ambao walipata nafasi ya kuchangia mada na
kuuliza maswali.
CHANZO: Ofisi ya waziri Mkuu
0 Maoni