The World-Residences at Sea, moja ya meli kubwa za kifahari
duniani na ambayo imekuwa ikizunguka dunia kwa miaka 20 sasa ipo Dar es Salaam,
Tanzania, muda huu unaposoma makala haya na imetia nanga leo Jumamosi Machi 30,
2024.
Meli hiyo ni tofauti na nyingine nyingi duniani kwani haina
abiria (passengers) bali ina matajiri takribani 400 ambao ni wamiliki
(residences) walioununua vyumba vyenye ukubwa mbalimbali katika meli hiyo na
hupanda kila mwaka kwenda kuzunguka maeneo mbalimbali ya dunia safari inayochukua
miezi mitatu kwa mzunguko mmoja.
Chumba kimoja hugharimu hadi Dola Milioni 2 (takribani TZS
Bilioni 4.5) ambapo nyumba kamili ndani ya meli hiyo yenye vyumba vitatu na
mambo mengine ya kifahari huuzwa kwa Dola Milioni mpaka 15 (Zaidi ya TZS
Bilioni 30).
Kazi kubwa ya kuitangaza Tanzania kupitia filamu ya
“Tanzania: The Royal Tour”iliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni
miongoni mwa mambo yaliyowavutia mabilionea wengi waliokuja na meli hiyo
iliyoanzia kutua Mafia, Zanzibar na sasa iko Dar mpaka kesho jioni. Baadhi ya
watalii hao wameruka kwa ndege kwenda kutalii maeneo mengine kama Serengeti,
Ngorongoro na Hifadhi ya Nyerere.
“Mimi binafsi nimekuwa nikivutiwa na Rais Samia na alipoingia
tu madarakani niliandika makala moja nzuri kumtambulisha duniani na katika
ulimwengu wa utalii. Nikavutiwa zaidi alipofanya filamu kuitangaza nchi. Nchi
yenu ina kila kitu mnapaswa kuitangaza zaidi,” anasema, Alain St. Ange, Waziri
wa zamani wa Utalii, Anga na Bandari wa Visiwa vya Seychelles, alipokutana baada
ya kushuka kwa muda kwenye meli hiyo akiwa mmoja wa watu waliokuja nayo na
kufanya mazungumzo na Dkt. Hassan Abbasi, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na
Utalii ya Tanzania juu ya namna ya kushirikiana nao jinsi ya kuitangaza zaidi
Tanzania na kuleta meli zaidi nchini na kupanua utalii wa fukwe, visiwa na
meli.
0 Maoni