Kufuatia baadhi ya Hospitali kusitisha huduma kwa wanachama
wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuanzia Machi 1, 2024, Uongozi wa
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) umekuja na mpango wa dharura wa kutoa huduma
kwa wanachama hao ili waweze kuwa na mwendelezo wa huduma hizo.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi amesema
hospitali imefanikiwa kuhamia kwenye kitita kipya cha mafao cha mwaka 2023
kilichopendekezwa na NHIF ambapo huduma zinaendelea kutolewa.
Prof. Janabi amesema, Hospitali imeongeza muda wa kuona
wagonjwa katika kliniki zote za Upanga kupitia vyumba 75 vya kuona wagonjwa na
vyumba vya kuona wagonjwa 59 viliyopo Mloganzila kuanzia saa tatu asubuhi hadi
saa nne usiku au mpaka mgonjwa wa mwisho atakapomaliza kuonwa na daktari.
“Tunajua kuna wagonjwa waliopangwa kufanyiwa upasuaji
(electives) tunavyo vyumba 18 vya upasuaji Upanga na Mloganzila vyumba vya
upasuaji 13. Kwa wagonjwa wenye tatizo la figo wanaohitaji kusafishwa damu,
Upanga tunazo mashine 47 za kutoa huduma hiyo na tumeongeza zamu (sessions) za
kutoa huduma hiyo katika mzunguko wa saa nne wa kila zamu kutoka tatu hadi nne
kwa Upanga na Mloganzila ambapo kuna mashine 12 tumeongezea mizunguko kutoka
miwili hadi minne na muda unaobaki ni wa kufanya matengezo kinga pamoja na usafi
wa mashine hizo,” ameeleza Prof. Janabi.
Prof. Janabi amesema MNH kama mmoja wa watoa huduma wakubwa
nchini nayo itaendelea kufuatilia utendaji wa kitita hicho ili kubaini
changamoto zitakazojitokeza na kuziwasilisha katika mamlaka husika.
0 Maoni