Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Nzega mkoani Tabora
imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela, Abdallah Seleman (37) aambaye ni Mwalimu
wa Madrasa katika Msikiti wa Ushirika baada ya kumtia hatiani kosa la kumlawiti
mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 12.
Katika hukumu hiyo Hakimu wa Wilaya hiyo Nasra Mwashee
amesema kuwa Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa mbele ya Mahakama pasina
shaka yoyote na kumuhukumu mtuhumiwa kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 30
jela.
Hakimu Mwashee amesema Mahakama imetoa adhabu hiyo ili iwe
fundisho kwake na watu wengine wenye tabia kama hizo au wenye nia ya kufanya
vitendo hivyo vya kikatili kwa watoto na kuongeza kuwa vitendo vya namna hiyo
vimekuwa vikitokea mara nyingi katika wilaya hiyo.
Upande wa Mawakili wa Serikali wakiongozwa na Jenipha Mandago
waliiambia Mahakama kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Oktoba 15, 2023 majira ya
saa 10 jioni baada ya kuwekewa mtego kutokana na malalamiko ya mara kwa mara
kutoka kwa watoto aliokuwa anawafundisha elimu ya dini katika msikiti huo.
Amessema kitendo cha kumlawiti mtoto huyo ambaye ni
mwanafunzi wa shule ya msingi Imeli Wilayani Nzega kilifanyikia chooni na
kumsababishia mtoto huyo maumivu makali.
Jenipha ameendelea kusema kuwa kutokana na uzito wa kosa hilo
waliiomba Mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine
wenye nia na tabia kama hizo kwenye jamii.
Kabla ya hukumu hiyo kutolewa hapo jana, Mahakama ilitoa
nafasi ya utetezi kwa mtuhumiwa iwapo itamtia hatiani ambapo aliomba apunguziwe
adhabu kwani anafamilia ya watoto wanne na mke ambao wanamtegemea.
Hata hivyo Mahakama haikuridhika na utetezi huo wa Abdallah
Seleman, na kumhukumu kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 30, ili iwe
fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
0 Maoni