Watu tisa wakwea kizimbani kwa mauaji ya mlinzi

 

Watu tisa wamefikishwa katika Mahakama ya wilaya ya Nyamagana kwa kosa la mauaji ya Yumen Elias [54] aliyekuwa mlinzi wa maduka katika eneo la Mwananchi kata ya Mahina wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza.

Akiwasomea shtaka hilo la mauaji namba 2665 la mwaka huu, Mwendesha Mashtaka wa Serikali George Ngemela amesema washtakiwa hao walitenda kosa hilo Januari 16 mwaka huu majira ya saa tisa usiku ambapo walimkata mlinzi huyo na kitu chenye ncha kali kichwani na kupeleka kufariki dunia.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya wilaya ya Nyamagana Juma Mpuya, Mwendesha mashtaka wa serikali George Ngemela amesema washtakiwa hao wametenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 196 na 197 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022, na kuwataja washtakiwa hao kuwa ni Julius Joseph [22], Charles Chacha [27], Leonidas Bukwimba [19], Poul John [23], Mussa Robert [22], Emanuel Makubi [18], Abdalah Hassan [31], George Mang’era [50] na Edward Boniface [19].

Washtakiwa wote tisa baada ya kusomewa shtaka hilo la mauaji hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza shtaka hilo na shtaka hilo litatajwa tena tarehe 20 ya mwezi huu, ambapo washtakiwa wakirudishwa rumande.



Chapisha Maoni

0 Maoni