WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Serikali
na sekta binafsi waweke mikakati ya kuhakikisha kuwa wanawake wanashiriki
kikamilifu katika fursa za uchumi wa kidijitali ili waweze kuongeza kasi ya
ukuaji wa uchumi.
“Viongozi wa Serikali, sekta binafsi, wadau wa maendeleo,
wananchi wekeni mikakati ya pamoja ya kukuza ushirikiano na kuwekeza kwenye
miundombinu ya TEHAMA ili kutoa kipaumbele katika kuongeza ujumuishi wa
kidijitali na wa kifedha.”
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Februari 15, 2024)
alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua mkutano wa
Future Ready Summit katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNICC), Dar es Salaam.
Katika mkutano huo ulioandaliwa na kampuni ya Vodacom,
Waziri Mkuu ametoa wito kwa makampuni ya simu yaweke gharama rafiki za
mawasiliano ili kuvutia washiriki wengi wakiwemo wanawake kushiriki katika
fursa za uchumi wa kidijitali.
Pia, Waziri Mkuu amewataka wadau wa sekta binafsi, watumie
majukwaa kama hilo la Future Ready Summit pamoja na kuandaa programu za
kuwawezesha vijana, hususan wakike ili nao waweze kushiriki katika kuchangia
uchumi wa Taifa.
“Kwenu washiriki wa mafunzo tumieni fursa hii vema,
shirikianeni na wawezeshaji, muwe na mijadala yenye tija ili mafunzo yawe na
tija inayotarajiwa. Aidha, mkawe mabalozi wazuri kwa wasichana na wanawake
kuhusu fursa zakidijitali na matumizi ya TEHAMA.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali inatekeleza mradi wa
ujenzi wa shule za sekondari 26 za kitaifa za wasichana mahsusi kwa masomo ya
sayansi ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwachochea wanafunzi wa kike wapende
masomo hayo.
Mheshimiwa Majaliwa amesema shule hizo zinajengwa katika
mikoa yote ya Tanzania Bara kwa gharama ya shilingi bilioni 104 ambapo ujenzi
wa kila shule moja inagharimu kiasi cha shilingi bilioni nne.
“Katika hili ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu
Hassan ambaye ni kinara wa kuhamasisha masuala ya sayansi, teknolojia na
hisabati. Hii ni kutokana na utashi wake
na hatua za makusudi alizozichukua kuhakikisha wasichana wanashiriki kikamilifu
katika fursa za masomo ya sayansi na hisabati.”
Awali, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari, Nape Nnauye alitumia fursa hiyo kuwaondoa hofu Watanzania juu ya
mapinduzi ya teknolojia na kuwataka wajipange na wasonge mbele.
Pia, Waziri huyo alisema jukumu la wizara hiyo ni
kuhakikisha kuwa uwekezaji unafanyika kwenye ujenzi wa miundombinu ya taasisi
na vyuo ambavyo vitafundisha masomo hayo. Alisisitiza kuwa Tanzania ipo tayari
kwenda mbele katika Mapinduzi ya kiteknolojia.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni