Kwa miongo kadhaa kumekuwa na dhana ya kwamba wageni wengi
wa nje hupendelea zaidi utalii wa kuona wanyamapori, lakini hivi karibuni dhana
hiyo imeanza kubadilika kwa kasi ambapo Tanzania imeanza kupokea wageni makundi
kwa makundi wakitembelea katika maeneo yetu ya Malikale hususan Hifadhi ya Urithi
wa Dunia ya Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.
Ni takrikani siku 9 sasa katika kipindi cha Mwezi Februari
kuanzia tarehe 03 - 11, 2024, Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania - TAWA imeweza kushuhudia
Meli zilizosheheni makundi ya Watalii kutoka Mataifa mbalimbali
zikipishana kutia nanga katika Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa
kisiwani na Songo Mnara na kufikisha idadi ya watalii wapatao 445 kwa safari
nne (4) za kitalii zilizofanyika.
Kwa mara nyingine Februari 11, 2024 TAWA ilipokea kundi la nne
(4) la watalii wapatao 114 kutoka Ufaransa ambao waliingia Kilwa kisiwani kwa
ajili ya shughuli za utalii na kufanya idadi ya watalii wa nje waliotembelea
hifadhi hiyo ndani ya siku 9 tu kuwa 445.
Hata hivyo, TAWA inategemea kuendelea kupata wageni wengi
kutoka Kona mbalimbali za Dunia kuja kutembelea na Kutalii Katika Hifadhi hiyo
kongwe yenye utajiri mkubwa wa kihistoria.
Kwanini Kilwa Kisiwani na Songo Mnara? Wahenga walisema ukitaka kuujua uhondo wa ngoma, uingie ucheze, hivyo TAWA inaendelea kuwakaribisha watalii wote wa ndani na nje kutembelea hifadhi hii kujionea yaliyomo.
Na. Beatus Maganja- Kilwa
0 Maoni