Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Dkt. Mehmet Gulluoglu amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa katika Ofisi za Wizara hiyo zilizopo
katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma ambapo wamejadiliana juu ya namna
ambavyo uhusiano wa kidiplomasia uliopo utazinufaisha nchi zote mbili katika
sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Akizungumza baada ya majadiliano hayo, Katibu Mkuu Msigwa
amesema yapo matumaini makubwa kwa nchi hizo mbili kufungua fursa mbalimbali
zinazogusa sekta hizo ikiwemo Wataalam wa lugha ya Kiswahili kufundisha lugha
hiyo nchini humo, kujenga kituo kikubwa cha utamaduni pamoja na kuendeleza miundombinu ya michezo
hapa nchini Tanzania.
“Kubwa ambacho Serikali ya Uturuki wako tayari ni kujenga
Kituo cha Utamaduni hapa Tanzania ili kutangaza tamaduni za pande zote mbili,
kuziendeleza na pia kutumia utamaduni kama fursa ya kiuchumi. Makubaliano
yakikamilika wako tayari kuanza na ujenzi wa kituo hicho,” amesema Katibu Mkuu
Gerson Msigwa.
Aidha, Katibu Mkuu Msigwa amesema Serikali ya nchi hiyo iko
tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika Sekta ya Sanaa ambapo
Wasanii wa Filamu kutoka nchini Tanzania watapata fursa ya kutembelea nchi hiyo
kujifunza zaidi kuhusiana na sekta hiyo na pia wasanii wa filamu wa nchi hiyo
kutembelea Tanzania ili kubadilishana uzoefu.
Kwa upande wa sekta ya michezo Msigwa amesema Serikali ya Uturuki imeonesha nia ya kutoa nafasi kwa timu za Taifa kuweka kambi katika nchi hiyo wakati wakati wa maandalizi ya michuano mbalimbali ya kimataifa.
0 Maoni