Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amekagua daraja la muda pamoja na
maandalizi ya ujenzi wa daraja la Mirumba lililopo kwenye jimbo lake katika halmashauri
ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.
Daraja hilo linaunganisha mkoa wa Katavi na Rukwa lina urefu
wa mita 60 na litagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 6.55.
Mhe. Pinda amekagua daraja hilo tarehe 22 Februari 2024
katika kata ya Mirumba ikiwa ni muendelezo wa kukagua shughuli za maendeleo
katika jimbo lake sambamba na maandalizi ya mkutano Mkuu wa jimbo hilo
unaotarajiwa kufanyika februari 24, 2024.
Akiwa katika eneo la daraja hilo, Mhe. Pinda ameoneshwa
kuridhishwa na ujenzi wa daraja la muda pamoja na maandalizi ya lile la kudumu
na kueleza kuwa, daraja hilo litakuwa suluhisho ya shida ya muda mrefu ya
wananchi wa Mirumba waliyokuwa wakiipata wakati wa mvua kubwa.
Mbunge huyo wa Kavuu amesema, anamuamini mkandarasi
aliyepewa kazi ya ujenzi wa daraja kutokana na kufanya kazi nzuri ya ujenzi wa
daraja la Mwamapuli-Chamalendi alilolieleza kuwa lina kiwango bora na sasa
limeanza kutumika.
‘’Mkandarasi! mimi sina tatizo na wewe na nina imani kazii
hii ya ujenzi wa daraja la Mirumba itafanyika vizuri na kwa ufanisi, nikutakie
kila la kheri,’’ alisema Mhe. Pinda.
Utekelezaji ujenzi wa daraja la Mirumba unafanywa na kampuni
ya ujenzi ya Safari General Business Co Ltd JV Advance na ni wa miezi 24.
Katika hatua nyingine Mbunge huyo wa jimbo la Kavuu
aliwatembelea vijiwe vya waendesha boda boda kwa lengo la kujua changamoto
zinazowakabili wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Akiwa katika vijiwa hivyo, Mhe. Pinda aliwataka waendesha
boda boda kuwa makini wakati wote wanapofanya kazi zao kwa kuwa umakini ndiyo
utakaowawezesha kuepukana na ajali zinazoweza kuepukika.
Aidha, Mbunge huyo wa Jimbo la Kavuu amewaahidi waendesha
bodaboda wa vijiwe vyote vya jimbo lake kuwapatia vizibao (Reflector) ili
wavivae wakati wote wanapofanya kazi zao.
Kwa upande wao, waendesha boda boda mbali na kumshukuru Mbunge wa kwa uamuzi wa kuwapatia Reflector walimuomba aangalie uewezekano wa kuwasaidia kupata mikopo ya pikipiki kutoka kwa kampuni zinazouza pikipiki. Mhe Pinda aliahidi kulifanyia kazi suala hilo.
Na. Munir Shemweta- Katavi
0 Maoni