Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro (NCAA) Jenerali Venance Mabeyo (Mstaafu) amepongeza kazi kubwa
inayofanywa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania kupitia SUMA-JKT kutokana na kazi
kubwa wanayoifanya katika ujenzi wa nyumba 2,559 katika kijiji cha Msomera
Wilayani Handeni mkoani Tanga.
Akizungumza kwa niaba ya wakurugenzi wa bodi wa Mamlaka
hiyo mara baada ya bodi hiyo kumaliza
ziara yao ya kikazi katika kijiji hicho Jenerali Venance Mabeyo (Mstaafu)
amesema kuwa kazi kubwa inayofanywa na jeshi katika ujenzi huo ni lazima iungwe
mkono na wadau wengine wa kisekta ili kukamilisha zoezi hilo haraka ili
wananchi waliojiandikisha kwa hiari kutoka ngorongoro waendelee kuhamia.
Amesema katika ziara hiyo bodi yake imejionea kusuasua kwa
baadhi ya sekta katika utekelezaji wa majukumu yao hivyo kushauri kila mdau ni
muhimu kuhakikisha anatekeleza majukumu yake.
“Jeshi mnafanya kazi kubwa ni muhimu sana kila mmoja wetu
atimize wajibu wake ili tuimarishe miundo mbinu ya kijiji hiki hasa nyumba ili
wananchi waweze kuhamia kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro,” aliongeza Mwenyekiti
huyo.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro Richard Kiiza amesema hamasa ya wananchi kuhamia katika kijiji hicho
ni kubwa ambapo mamlaka itaendelea kuwahamisha kadri wanavyojiandikidha.
Kaimu Operesheni Kamanda wa mradi huo Luteni kanali Edward
Mwanga aliwahakikishia wakurugenzi hao wa bodi kuwa ujenzi wa nyumba hizo
utakamilika kutokana na kasi na ari ambayo wanayo katika utekelezaji.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Handeni mhe. Albert Msando amesema wataendelea kuwapokea wananchi wanaotoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ili kutimiza azma ya serikali ya kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na maisha bora.
0 Maoni