WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwakilisha Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwenye mkutano wa dharura wa nchi wanachama wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika kwa njia ya mtandao.
Mkutano huo uliofunguliwa na Rais wa Angola, Joao Manuel
Lourenco ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, ulikuwa na ajenda moja tu ya
kujadili kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika ukanda wa SADC.
Akizungumza kutoka ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma leo
(Ijumaa, Februari 02, 2024), Waziri Mkuu Majaliwa amesema Tanzania inapendekeza
kuwa ni vema Kanda ya SADC ikachukua hatua jumuishi kwa kuhusisha sekta zote
mtambuka ikiwemo sekta za maji na mipango miji ili kuleta suluhisho la kudumu
la kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu na magonjwa mengine ya mlipuko.
“Hii ni kwa kuzingatia kuwa jamii kwa ujumla na kila
mwananchi ana jukumu la kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha anazingatia kanuni
za usafi (WASH) kwa manufaa binafsi, jamii na ukanda mzima.”
“Tunashauri nguvu kubwa ielekezwe katika kuboresha mifumo na
upatikanaji wa maji safi na salama katika jamii zetu ili kuwa na matokeo chanya
katika kudhibiti mlipuko huu.”
Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu;
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk.
Mapema, akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa SADC, Rais
Lourenco alisisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuimarisha mawasiliano baina ya
wataalamu wake ili kusaidiana kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo hasa kwenye
maeneo ya mipakani.
Aidha, alisisitiza viongozi wa nchi wanachama waweke
kipaumbele kwenye teknolojia mpya na tafiti ili kukabiliana na magonjwa ya
mlipuko. “Ni lazima tuhakikishe mifumo yetu ya afya inaweza kukabili na
changamoto hizi za magonjwa ya mlipuko.”
Marais walioshiriki mkutano huo ni Phillipe Nyusi
(Msumbiji), Lazarus Chikwera (Malawi), Emmerson Mnangagwa (Zimbabwe), Haikande
Hichelema (Zambia) Felix Tshisekedi (DRC). Wengine ni wawakilishi wa Wakuu wa
Nchi kutoka Afrika Kusini, Lesotho, Eswatini, Seychelles na Madagascar.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni