Hamasa ya wananchi wanaojiandikisha kuhama kwa hiyari kutoka
eneo la hifadhi ya Ngorongoro imeongezeka ambapo leo tarehe 19 February , 2024
jumla ya kaya 82 zenye wananchi 541 na mifugo 3,379 zimehama kutoka Ngorongoro
kweda Kijiji cha Msomera Handeni Tanga.
Akizungumza wakati wa kuaga kundi hilo Kamishna wa Uhifadhi
wa NCAA Richard Kiiza amesema kuwa baada ya kuhama kwa kundi hilo leo inafanya
idadi ya wananchi waliokwishahama ndani ya hifadhi tangu zoezi lilipoanza hadi
leo kufikia kaya 1,032 zenye watu 6,395 na mifugo 28,982.
Kamishna Kiiza amebainisha kuwa kadri siku zinavyoenda
wananchi wengi wanahamasika na kujiandikisha kuhama kwa hiari yao wenyewe hasa
baada ya ushuhuda wa maisha mazuri kwa wananchi wenzao waliokwishatangulia
ambao Maisha yao yamebadilika kwa kiasi kikubwa.
“Wananchi waliotangulia mwaka jana wengi wao wamejenga
nyumba za kisasa, wamelima mazao ya kutosha kwa ajili ya chakula na biashara,
wanamiliki vyombo vya usafiri, wanapata huduma bora za maji, umeme, shule,
mawasiliano, huduma za afya, posta, malisho na majosho, hali hii imefanya wao
kuwa mabalozi kwa wenzao waliobaki Ngorongoro,” ameongeza Kiiza.
Kiiza ameongeza kuwa wananchi ambao walikuwa
hawajajiandikisha wamegundua walikuwa wanapotoshwa na baadhi ya watu ambao
hawaishi ndani ya hifadhi, bila kujua changamoto wanazokutana nazo wananchi za
kushambuliwa na Wanyama wakali na kushindwa kufanya baadhi ya shughuli za
kiuchumi kutokana na sheria za hifadhi.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Kanali Wilson
Sakulo akiwaaga wananchi hao ameeeleza kuwa wananchi wote wanaohama haki zao za
msingi zimezingatiwa kwa mujibu wa sheria, na kila kaya inayoondoka inaingiziwa
fedha kiasi cha shilingi milioni 10 na fedha zingine za fidia ya maendelezo
waliyoyafanya wakiwa Ngorongoro.
Amewahakikishia wananchi hao kubwa mbali na faida na huduma wanazozikuta msomera wakiwa safarini pia Serikali inawapatia ulinzi na escort , huduma ya afya, chakula cha njiani, kusafirishiwa mizigo yao na mifugo yao na wakifika Msomera watakabidhiwa nyumba ya vyumba vitatu iliyoko kwenye eneo la ekari 2.5, shamba la ekari 5 na kupewa mahindi ya chakula kwa kipindi cha miezi 18.
Na. Mwandishi wetu- NCAA
0 Maoni